Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeanza kuwasakama madiwani wanaodaiwa kukisaliti katika Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Katika uchaguzi wa meya uliofanyika Desemba 16, mwaka jana madiwani wawili wa chama hicho walidaiwa kukisaliti na kumpigia kura mgombea wa CCM, Priscus Tarimo. Hata hivyo, katika uchaguzi huo uliokuwa na wajumbe 30, mgombea wa Chadema, Raymond Mboya aliibuka kidedea kwa kupata kura 22, huku Tarimo akipata tano.Tafsiri ya matokeo hayo ni kuwa kama madiwani wa CCM katika baraza hilo wako watatu na mgombea wao alipata kura tano, ni wazi madiwani wa Chadema walimpigia.

Wiki iliyopita Kaimu Katibu wa chama hicho katika manispaa hiyo, John Minja aliwaandikia barua madiwani wanaodaiwa kufikia watano wakituhumiwa kuhusika na usaliti huo na kutaka wajieleze.

“Baada ya kusoma taarifa ya kamati ya uchunguzi imeonekana wewe ni mmoja kati ya madiwani waliokisaliti chama wakati wa uchaguzi wa meya na naibu meya,” ilisomeka sehemu ya barua waliyopelekewa.

Barua hiyo ilitumwa kwa madiwani hao kila mmoja na nakala yake, ikidai kitendo hicho kilikiuka katiba ya chama na kanuni za madiwani wa Chadema ibara ya 5.0 vifungu vidogo vya (a) na (c).

“Kamati ya utendaji kwa mamlaka iliyonayo inaagizwa kuleta utetezi wako ndani ya siku 14 kuanzia tarehe unapopokea barua hii. Mwisho wa kupokea utetezi ni tarehe 04.02.2016,” ilisema barua hiyo. Hata hivyo, baadhi ya madiwani wanadai kuwapo kwa mpango mahususi wa kuwaondoa wasiomnyenyekea mmoja wa viongozi, jambo ambalo hawatakubali.

“Kwanza kura zilipigwa kwa siri, hivi unajuaje nani alimpigia nani? Hiki kinachofanyika ni kututisha lakini hatutabadilika na tunazijua vizuri haki zetu,”alidai mmoja wa madiwani hao.

Madiwani hao ambao waliomba majina yao yasitajwe walidai hata uamuzi wa kumsimamisha Katibu wa Chadema wa manispaa hiyo, Steven Buberwa ni mwendelezo wa kukigawa chama.

Mwenyekiti wa Chadema Manispaa ya Moshi ambaye pia ni Mbunge wa Moshi Mjini, Jaffar Michael alisema bado hawajafikia hatua za kuwachukulia hatua madiwani na kinachoendelea ni uchunguzi.