98% ya wazanzibar ni waislam. Hivi kwanini wanahasimiana, wanagombania madaraka?
Hivi wanaamini wataishi milele? Wanaamini kwamba ukiwa na cheo duniani ndio utahama nacho?
Hawajosma na hawapitii quran? hakusoma madrasa?
Tungalie maisha ya watu wa peponi na maisha ya watu wa motoni baada ya binaadamu kufa


MAISHA YA WATU WA PEPONI

Pia ndani ya Bustani hii nzuri isiyo na mfano wake patakuwa na majumba ya ghorofa mazuri yasiyo na mfano na yenye fanicha nzuri zisizohadithika. Maalezo ya Qur-aan na Hadiyth katika kuelezea uzuri wa Pepo ni kama mfano tu kwani vipaji hivi vya ufahamu tulivyonavyo ni vya hapa hapa duniani tu na havina uwezo kabisa kuviingiza katika picha sahihi ya matukio yote ya maisha ya Aakhirah. Katika maisha hayo ya Aakhirah watu watakuwa na maaumbile na vipaji vinavyolingana na maisha hayo na kila mja ataona na kuhisi maisha ya huko kwa uhakika. Hivi ndivyo anavyotufahamisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth ifuatayo:
Kutoka kwa Abu Hurayrah amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema:
“Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) kasema: Nimemuandalia mja Wangu mema ambayo hapana jicho lilowahi kuona, Na hapana sikio lilopata kusikia, Na hapana moyo wa mtu uliopata kufahamu (kufikiri). Na sema kama unapenda. “Nafsi yoyote haijui iliyofichiwa katika hayo yanayofurahisha macho (huko Peponi) ni malipo ya yale waliyokuwa wakiyafanya” [32: 17]”. [Al-Bukhaariy na Muslim].

Kwa maana ya ujumla, Neno ‘Al-Jannah’ limetumiwa katika Uislamu kama kielelezo cha mazingira mazuri katika maisha ya Aakhirah ambapo watu wema walioishi hapa duniani kwa wema, kwa kufuata barabara kanuni za maisha ya siku kama zilivyowekwa na Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala), Waishi milele kwa furaha na amani. Hali ya mazingira ya maisha ya wenyeji wakazi wa Peponi inafafanuliwa katika Hadith zifuatazo:

Jaabir (Radhiya Allaahu ‘anhuma) amesimulia kuwa, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: “Hakika wakazi wa peponi watakula na kunywa lakini hawatakuwa wanatema, Wala hawendi haja ndogo au kubwa, Wala kutokuwa na uchafu puani. Waliuliza Maswahaba: kitakuwaje chakula? Alijibu Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) kitakuwa kitamu kama utamu wa miski na watakuwa wamejazwa na Tasbihi na Tahmidi kama walivyojaaliwa kupumua.” [Muslim].

Pamoja na Hadiyth hizi, Pia tuangalie na Qur-aan inasemaje juu ya maisha ya Peponi pamoja na wakazi wake na sifa zitakazotuwezesha kuingia katika Pepo.

“Kwa yakini watu wa Peponi leo wamo katika shughuli (zao), Wamefurahi. Wao na wake zao wamo katika vivuli, Wameegemea katika viti vya fahari. Watapata humo (kila namna ya) matunda na watapata kila watakavyovitaka. Salama (tu juu yao), ndio neno litokalo kwa Mola (wao) Mwenye Rehema.” [Yaasiyn: 55-58]

Na Amesema Aliyetukuka:

“Sema: “Nikwambieni yaliyo bora kuliko hivyo? Kwa ajili ya wamchao Allaah zipo Bustani kwa Mola wao, Zipitazo mito mbele yake.

Watakaa humo milele na wake (zao) waliotakaswa (na kila uchafu na kila ubaya). Na wana radhi ya Allaah na Allaah Anawaona (wote) waja (Wake).”

Ambao wanasema: Mola wetu! Hakika sisi tumeamini basi tughufirie madhambi yetu, na utuepushe na madhambi ya moto” Wafanyao subira na wasemao kweli na watiio na watoao (sadaka) na waombao maghfira saa za karibu na Alfajiri.” [Al-‘Imraan: 15-17]

Hebu tuangalie ni furaha ilioje kwa Mume na Mke watakapokutana katika Pepo ya Allaah na kuyaendeleza Maisha yao kwa raha kamili ambayo haina mfano? Ni raha ilioje hiyo jamani? Pia Ni raha ilioje kukutana na watoto wako katika Al-Jannah na kujumuika pamoja? Na pia kukutana na Ndugu na Jamaa huko ni Raha ilioje? Jamani ndugu zangu tujitahidi katika kuitafuta Pepo na si kuihangaikia hii dunia isiyokuwa na manufaa kwetu.

Enyi waja wa Allaah tushikamane na ‘Ibaadah ili tuweze kufaulu kuipata Pepo yake Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) kama Alivyotuahidi Mwenyewe, Tusihadaishwe na mapito ya dunia kwani hakika Mola Wetu Ametuandalia Maisha maradufu yasiyo na mfano kwa mwenye kufaulu kwa kumcha Yeye Pekee Bila ya kumshirikisha, kwa hiyo tushikamane na ‘Ibaadah ya kumuabudu Allaah na kufuata yote Aliyokuja nayo Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Na kuacha aliyotukataza. Tunamuomba Allaah Atuongoze na Atujaalie tuwe ni wenye kuipata Al-Jannah, Aamiyn.MAISHA YA WATU WA MOTONI

“Na bila shaka Jahannamu ndipo pahali pao walipoahidiwa wote. Ina milango saba; na kwa kila mlango iko sehemu walio tengewa”. [Suratu-Al-Hijr:43-44].
“Atauingia Moto wenye mwako”. [Suratul-Masad: 3].
“Hasha! Atavurumishwa katika Hutwamah”. [Suratul-Humazah: 4].
“Basi wapo miongoni mwao waliyoyaamini, na wapo walioyakataa. Na Jahannam yatosha kuwa ni (Sa’iyra) moto wa kuwateketeza”. [Suratun-Nisaa: 55].

“Hakika hiyo (Jahannaam) ni kituo kibayana mahali (pabaya kabisa) pa kukaa (hata kwa muda mfupi.” [Suratul-Furqaan: 66]
Pia tuone anavyotufahamisha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya kiwango wa adhabu ya motoni.

Nuuman bin Bashiyr amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema; “Hakika atakayekuwa na adhabu nyepesi kabisa katika wakazi wa motoni ni yule atakayekuwa na viatu vya moto, Kwa moto huu, (wa miguu utachemsha ubongo wake kama maji yachemkavyo kwenye birika). Haitaonekana kuna kiwango cha chini kabisa cha adhabu.” (Al-Bukhaariy na Muslim).


Kwa ujumla moto wa adhabu alioandaa Allaah (Subhaananu Wa Ta’ala) kwa watu waovu ni mkali sana.

Ndani ya mazingira ya motoni patakuwa na miti michungu, Na mti maarufu kwa uchungu ni “Zaqquum”. Tunapata maaelezo kamili ya mti wa “Zaqquum” ambao umeenea katikati ya Jahannam na watakaostahiki kuula ni katika Aayah zifuatazo:

“Je! Kukaribishwa hivi si ndio bora, au mti wa Zaqquum?

Hakika Sisi tumeufanya huo kuwa ni mateso kwa waliodhulumu.

Hakika huo ni mti unaotoka katikati ya Jahannam.

Mashada ya matunda yake kama kwamba vichwa vya mashetani.

Basi hakika bila ya shaka hao watayala hayo, na wajaze matumbo.

Kisha juu yake wanyweshwe mchanganyo wa maji yamoto yaliyo chemka.” [Asw-Swaffaat: 62-67].

Na katika Suratul-Fajr:

“Na ikaletwa Jahannamu siku hiyo, siku hiyo mtu atakumbuka! Lakini kukumbuka huko kutamfaa nini?

Atasema: Laiti ningeli jitangulizia kwa uhai wangu!

Basi siku hiyo hataadhibu yeyote namna ya kuadhibu kwake.

Wala hatafunga yeyote kama kufunga kwake.” [Suratul-Al-Fajr: 23-26].