SIKU 50 tangu Rais John Magufuli aingie madarakani, kuna mambo aliyafanya kwa vitendo ambayo bila shaka yamegusa nafsi za wananchi, hasa kuonyesha kwamba anawajali wananchi wa hali ya chini na pia kuhakikisha watendaji wanawajibika kwa vitendo vyao.
Nadhani hili lilikuwa muhimu kuonyesha kwamba mambo hayataenda kama ilivyozoeleka katika awamu yake na kwamba awamu yake ya tano ni kitabu kipya, ni tofauti na awamu tatu zilizopita. Sitaki kulinganisha na Awamu ya Mwalimu Nyerere, kwa hiyo hatua alizochukua zinaonyesha hilo.
Lakini pia katika kipindi hiki ametoa hotuba mbili, hotuba moja alitoa wakati anazindua Bunge, katika hotuba ile ingawa ilikuwa ni nzuri, aliorodhesha maovu ya jamii yetu na utawala wetu na jinsi atakavyokabiliana na maovu hayo.
Lakini hotuba iliyonifanya mimi kama mwanazuoni kuona kwamba inaonyesha mwelekeo wake na hasa dhamira ya wapi anakwenda, anaongozwa na dira gani, ni hotuba aliyoitoa kwa wafanyabiashara Desemba 3, 2015.
Kwangu mimi kama msomi hotuba ile ina umuhimu wa kipekee na kwa kiasi fulani inashangaza kwamba haijajadiliwa sana kwa sababu nafikiri watu bado wako katika mshangao wa vitendo alivyofanya. Mimi ningependa kuangalia kwa undani kidogo hotuba ile aliyotoa kwa wafanyabiashara, kwa sababu inatupatia mwelekeo na mtazamo wake.
Inawezekana mambo bado hayajaiva, bado yanapikwa lakini kwa kiasi fulani tunaweza kuainisha anakotaka kuelekea katika awamu yake, baada ya kufanya uchambuzi wa hotuba ile ninaona kuna mambo matatu muhimu amegusia.
Kwanza ana mwelekeo wa kujenga uchumi wa kitaifa (national economy), pili anataka kudhibiti uporaji wa rasilimali na mtaji wa nchi hasa rasilimali zinazoporwa na kusafirishwa nje bila wananchi kufaidika, na tatu ameonyesha haridhiki na sekta ya fedha, haya mambo matatu mimi nimeona kwenye hotuba yake.
Kwanza tukumbuke kuwa alikuwa anazungumza na wafanyabiashara kutoka sekta binafsi, alikuwa anazungumza na wawekezaji wa ndani. Katika mazungumzo hayo, alisisitiza kwamba wawekezaji wa ndani wana nafasi katika kujenga uchumi wetu na nchi yetu na yeye, pamoja serikali yake itashirikiana nao.
Lakini hakumalizia hapo tu, aliainisha sifa za hao wawekezaji wa ndani, matarajio yake ni nini kutoka kwa hao wawekezaji wa ndani au tuite kwa jina lake mabepari wa ndani, nimeona katika hotuba yake amerudia kwa kusisitiza angalau bepari yeyote popote duniani anaongozwa na kuchuma faida, huu ni ukweli, lakini yeye angepeda kuona mabepari wanakuwa mabepari wa kizalendo, wa kitaifa (national bourgeois), watakuwa wanatanguliza maslahi ya Watanzania mbele, alikuwa anasisitiza angependa kuona tabaka hili liwe la mabepari wa kitaifa.
Mabepari wa kitaifa
Mabepari wa kitaifa wanazo sifa tatu au nne hivi, na yeye ingawa hakuweka katika maneno yake lakini aligusia, moja ni kwamba hawa wanajikita katika uzalishaji siyo uchuuzi tu, yaani kununua bidhaa na kuuza kwa bei zaidi, siyo wachuuzi - ni wazalishaji wanawekeza katika sekta ya uzalishaji, hii ni moja, na hii ni muhimu kwa sababu wengi tunaowaita sisi wawekezaji hasa wa ndani siyo wawekezaji kwa sababu hawajajikita katika uzalishaji, wamejikita zaidi katika uchuuzi au kuuza bidhaa na Mwalimu Julius Nyerere alilizungumza vizuri sana suala hili, mwaka 1989.
Mwalimu pia alikuwa anazungumza na wafanyabiashara na watendaji wakuu wa serikali wakati ule. Ninavyoona kwenye hotuba hii ya Rais Magufuli, kuna mambo ambayo unaweza kuyalinganisha na yale aliyozungumza Mwalimu Nyerere mwaka 1989, pamoja na yale aliyokuwa akizungumza Marehemu Edward Sokoine mwanzoni mwa miaka ya 1980, haya yote yamejitokeza katika hotuba yake.
Kuhusu wazalishaji na wachuuzi, Mwalimu Nyerere alisema na ningependa kumnukuu hapa kwa sababu ameeleza vizuri tu; “Kwa Coca Cola, kwa sababu Marekani ana nguvu sana kwa Coca Cola, Marekani sasa anataka wote tuwe tunakunywa Coca Cola, ndugu Mengi mpende msipende mtatuuzia tu Coca cola. Kwa hiyo tunajivunia huo ugonjwa wala hatuoni haya, una-parade silaha za wakubwa, una-parade madege ya wakubwa, una-parade bidhaa za wakubwa, una-parade ma coca cola ya wakubwa na unajivuna tu sisi tumeendelea.”
Na Rais Magufuli kwa maneno yake anasisitiza uzalishaji wa bidhaa, hii ni sifa mojawapo na amegusia. Sifa nyingine ya tabaka hili kutumia malighafi ya nchi ili kutengeneza bidhaa kwa ajili ya mahitaji ya ndani. Anatengeneza bidhaa kwa mfano kwenye kiwanda ili kukidhi mahitaji ya ndani, Kiingereza wanasema kuna kuwa na “backward and forward linkages” ndiyo maana hasa ya kiini cha kujenga uchumi wa kitaifa, hii ni sifa ya pili.
Kwa nini nasema Rais Magufuli ana mwelekeo huu, ametoa mifano kama mitatu hivi kwanza ametoa mfano wa ngozi, kwamba nchi ya Tanzania ina mifugo mingi katika Bara la Afrika, ya pili baada ya Ethiopia kuwa na mifugo mingi, lakini hatuna viwanda vya ngozi, hatutumii mifugo yetu kuwa na ngozi za kutegeneza viatu kwa ajili ya soko la ndani. Kama unakumbuka inawezekana vijana wamesahau, tulianza hiyo, tulikuwa na viwanda vya ngozi Morogoro, baada ya kuingia kwenye mfumo wa uliberali mambo leo na kufungua milango, viwanda vyote vilikufa vingine vilibinafsishwa sasa ni magodown na Rais Magufuli amezungumzia hilo.
Mfano wa pili anaoutoa ni kwamba mazao yanayotokana na mifugo, mfano maziwa, samli, siagi hatutengenezi sisi kwa ajili ya soko letu, mfano mwingine aliotoa ni wa mbao, tuna mapori hapa lakini magogo yanasafirishwa tu kwenda nje.
Hatutumii hayo magogo kutengeneza samani, tunaagiza kutoka nje na utakumbuka amepiga marufuku kwamba samani katika ofisi za serikali lazima zinunuliwe hapa hapa, mfano wa tatu ni ule wa samaki na ameeleza vizuri tu kwa nini sisi tusiweze kuchakata samaki zetu kwa ajili ya soko letu, ameeleza hapa ningependa kunukuu faida ya kuwa na mwelekeo kama huu; “Mtu anayevua samaki kwenye maji marefu kule baharini na kuleta hapa, akawa ana wachakata mwenyewe kwenye viwanda vyake anasafirisha hawa samaki aina ya tura kupeleka hata Ulaya, watu wetu wa hapa wakapata ajira, serikali ikapata mapato yake na mabaki ya samaki yakatumika kutengeneza hata chakula cha kuku huku naye akijipatia fedha zake na maisha yakaendelea.”
Anawaambia hawa wawekezaji wa ndani kwa nini ninyi msifanye kazi hiyo, badala ya kuwaachia watu wa nje wavue samaki wetu na kupeleka nje? Unaona hapa kuna mwelekeo wa zile sifa za mabepari wa kitaifa kujenga uchumi wa kitaifa. Kutokana na mifano hii anayotoa ninavyoona mimi mwelekeo wake juu ya mfumo wa uchumi ni kujaribu kuchukua hatua za makusudi kabisa kujenga uchumi wa kitaifa. Na katika hili, anasisitiza kwamba nyie wawekezaji wa ndani mngekuwa na sifa hizo za mabepari wa kitaifa, ndiyo maana ya kusema kwamba wekeni maslahi ya Watanzania mbele msiwe wachuuzi tu.
Siku 50 za Rais Magufuli
Siku 50 ni chache sana kuwa na mwelekeo wa vitendo, kwa sababu kama nilivyosema, ndiyo maana nimejikita kwenye hotuba yake, hii inaonyesha mwelekeo, lakini sasa atafanyaje, atachukua hatua gani katika mfumo wenyewe ili kuelekea huko, kujenga uchumi wa kitaifa na baadaye nitazungumzia kama kweli umeamua kujenga uchumi wa kitaifa kunakuwa na masharti yake.
Lakini kwa sasa inaonyesha dhamira yake ni kujenga uchumi wa kitaifa, na hili ndiyo alikuwa anawaambia wawekezaji wa ndani muwe na sifa za kusaidia kujenga uchumi wa kitaifa na mkifanya hivyo sisi serikali tutawasaidia, tutawawekea mazingira .
Kwa mfano amezungumzia kuweka mazingira, kupunguza kodi za kero kwa wafanyabiashara wa kati na wadogo, lakini pia ameweka masharti mengine na ndiyo sifa mojawapo kwamba huwezi ukakwepa kulipa kodi.
Hii ni sehemu ya kwanza, sehemu ya pili ameonyesha kuwa anakasirishwa sana na uporaji, katika hili pia ameonyesha kwa kiasi fulani wako mabepari wazawa ambao siyo mabepari wa kitaifa, kwa Kiingereza hawa tunawaita “ma-comprador,” isipokuwa yeye mwenyewe hakutumia neno hili, lakini kulikuwa na jambo moja amezungumzia kwa kiasi fulani linaonyesha yeye anasisitiza tabaka la mabepari wa kitaifa lisiwe tabaka la wachuuzi linalotaka kupora rasilimali na kupata faida haraka haraka kwa kusaidiana na waporaji wa nje.
Kwa mfano anasema; “..nafahamu Mwanyika yuko hapa (Mwanyika ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu) kwenye madini kule kuna ndege zinatua kila siku, sina uhakika vile vyote vinavyobebwa na ndege hizo tunavijua, lakini kwa kuwa nafahamu wewe ni Mbena au sijui ni Mhehe na mna tabia ya kujinyonga kila mambo yanapoharibika basi simamia haya mambo vizuri”.
Hii ninaona ni ishara kwamba mimi sitaki mabepari ambao watashirikiana na waporaji wa nje kufaidika wao wenyewe, kwa mfano wale ambao wameng’ang’ania sana wazawa wapewe vitalu vya gesi ili wao sasa wawe na ubia na watu wa nje, sasa kama ni hivyo kwa nini serikali yenyewe isiwe na ubia na watu wa nje ili iweze kuthibiti. Badala ya kuwekeza kwenye viwanda na kujenga ajira, kama nilivyosema kutumia malighafi ya ndani kukidhi mahitaji ya ndani kwa nini huyu mwekezaji ang’ang’anie sana kupata kitalu kwa sababu yeye ni mzalendo wakati yeye hazalishi chochote, atafunga mkataba na watu wa nje waje kupora rasilimali zetu.
Na hii pia amezungumzia kwa sababu sifa mojawapo ambayo amesisitiza sana Magufuli ni kwamba uwekezaji katika uzalishaji hasa viwanda uweze kujenga ajira, kama wewe ni mwekezaji utaweka mitambo ya aina gani, kwa mfano, ili kuhakikisha kwamba unaweza ukapanua ajira na hii aliizungumzia Rais, akizungumza na Reginald Mengi, akazungumzia suala la ajira na anamnukuu anasema wakati anatoa mfano huu, Mengi, wakati anatoa mfano huu alikuwa anajisifia kwamba sekta ya viwanda kwa sasa imetoa mchango mkubwa wa ajira kwa taifa hili kwa kuajiri watu laki moja.
Rais Magufuli anasema wizara niliyokuwa mie, Wizara ya Ujenzi ilikuwa na ajira ya watu milioni 1.3, wizara moja tu ya serikali, sasa nyie kwenye viwanda mia nne mnasema mmetengeneza ajira lakini moja tu, anasema hii ni ajira ya aina gani, na ukweli ndivyo ulivyo, tulikuwa na wafanyakazi wameajiriwa katika sekta ya viwanda kabla ya ubinafsishaji zaidi ya laki tatu sasa leo hii tunajisifia kwa kuwa na ajira ya watu laki moja, hata wafanyakazi wa nyumbani ni mara nne na zaidi kuliko hao, hapo hatujafanya chochote cha kujisifia kwamba umejenga ajira ya watu zaidi ya laki moja. Na hapa amesisitiza sana kwamba uwekezaji katika sekta ya uzalishaji na viwanda utengeneze ajira kwa ajili ya vijana wetu.
Sekta ya fedha
Jambo la tatu ni sekta ya fedha, yeye hakupanua sana lakini nimekuta hapa jambo moja alilozungumzia ambalo liko wazi lakini halizungumziwi, kwa sababu tusisahau tulivyobinafsisha, tulibinafsisha sekta ya fedha - benki, bima na anasema hapa Rais Magufuli, “…kwenye sekta ya benki kwa mfano Dk. Kimei anafahamu, tunazo benki kubwa karibu 54 na zote zinafanya kazi na serikali, na zote hizi hazijajikita chini kwenda kwa wananchi juzi hapa tumejaribu kufanya uchambuzi na tukakuta karibu shilingi bilioni 550 zinazozunguka katika benki hizi ni pesa za umma, ambazo kiukweli ni pesa za serikali zinazotokana na mfumo wa hati fungani, kwa hiyo kwa maana nyingine serikali inafanya biashara na mabenki haya kwa kutumia fedha zake yenyewe.”
Miaka michache iliyopita mfanyakazi mmoja wa Benki Kuu aliwahi kuniambia, baada ya kubinafsisha mabenki, hela zote za mishahara ya wafanyakazi wa serikali ambao wako nchi nzima zinawekwa kwenye NBC, kwenye mabenki ya watu binafsi na mshahara unalipwa mwisho wa mwezi, katika kipindi hiki cha mwezi mmoja mabenki wanatumia hela hizo kununua Treasure Bond (hati fungani) na kupata riba kwa hela hizo hizo za serikali. Mabenki haya katika hesabu zao wanaonyesha wana deposit kubwa sana imewekwa kwa fedha zetu lakini Watanzania hawakopesheki, kwa hiyo hawapati mikopo, hela hizo zinakwenda wapi?
Tunasema nchi hii ni masikini, na mimi nimerudia rudia sana kuzungumza hili, kama nchi hii ni masikini haya mabenki yote yanafanya nini hapa? Hela hizo zinatoka wapi, kwenye sekta ya fedha kuna mabenki kuna bima, siku hizi ulimwenguni bima ni taasisi kubwa sana ya kulimbikiza mtaji. Kwa hiyo alitaka kumaanisha kwamba kuna kitu hakiko sawa, ingawa kama nilivyosema mawazo yake bado hayajapikwa vizuri, bado anafikiria, katika kutoa mfano huu nafikiri anawaza katika sekta yetu ya fedha kuna walakini inabidi tufikirie vizuri.
Na mimi ningeongeza siyo mabenki tu, taasisi nyingine za fedha kama bima, akiba za uzeeni, taasisi hizi zinalimbikiza mtaji mkubwa sana, ingetusaidia sana kama tungeweza kutumia mtaji huu katika kuwekeza kwenye viwanda kwenye kilimo, lakini sasa huwezi ukafanya hivyo kama hudhibiti haya mabenki, bima kama dhana ya soko huria umeweka mikononi mwa watu binafsi, akiba za uzeeni zinalimbikiza hela nyingi sana lakini kama hatuna mpango wa uwekezaji wa dhati kabisa hasa katika uzalishaji, mtaji huu unaondoka tu au unawekwa kwenye sekta ambazo hazizalishi ajira wala haziendelezi uchumi.
Ujenzi wa uchumi wa kitaifa
Mimi ningesema kwamba ukitaka kujenga uchumi wa kitaifa, jambo la kwanza kabisa huwezi ukaachia uchumi wako kwa soko huria, lazima uwe na mpango wa kuelekeza uchumi huo kwenye uchumi wa kitaifa, kwa hivyo kuna sekta muhimu na nyeti tatu ambazo lazima uzidhibiti ama kwa kumilikiwa na serikali moja kwa moja au zidhibitiwe kwa karibu sana.
Sekta ya kwanza ni sekta ya fedha, kwa sababu ukitaka kujenga uchumi wa kitaifa lazima udhibiti sera ya fedha, hii huwezi ukawaachia watu binafsi. Sekta nyingine nyeti sana ambayo lazima iwe mikononi mwa serikali ni nishati yaani umeme, maji, rasilimali na mapori. Sekta ya nishati lazima iwe mikononi mwa serikali huwezi kuachia watu binafsi.
Sekta ya tatu ni ardhi, rasilimali zote zinazopatikana chini ya ardhi na juu ya ardhi huwezi kuachia watu binafsi. Kwa hiyo sekta hizo nyeti ama unazidhibiti kwa karibu sana au unaziacha mikononi mwa serikali. Chini ya hiyo ndiyo unajenga uchumi wako, unawaachia mabepari wa ndani wawekeze kwenye viwanda, na hapa kuna viwanda vikubwa sana ambavyo serikali inaweza ikashiriki, na vya kati na hali ya chini hawa unawawekea mazingira mazuri ili wakidhi mahitaji ya ndani, watumie malighafi ya ndani. Kwa maoni yangu kwa hotuba ile na yale aliyozungumzia ni kama anataka kujenga uchumi wa kitaifa. Hayo aliyozungumzia hayawezekani kama huna lengo hilo na hukidhi masharti yake, kwa mfano ukiwajengea mazingira tabaka lako la ndani la mabepari wa kitaifa kuna mambo mawili kutoka juu, moja walipe kodi pili wawekeze kwa malengo yanayowekwa na serikali.
Unapokuja serikalini kuomba kibali kutakuwa na vigezo. Je, utatumia malighafi ya ndani? Utazalisha bidhaa ambazo ni mahitaji ya watu wa ndani? Utatumia mitambo ambayo itaongeza ajira?
Ingawa serikali haimiliki viwanda lakini ina vigezo, kabla kumruhusu huyu kwenda kuwekeza na si jambo geni ndivyo zilivyofanya nchi za Korea Kusini na Taiwan, ndivyo walivyofanya kunakuwa na mpango kabisa, ingawa uchumi hauko mikononi mwa serikali lakini wana mpango.
Haya ni masharti mawili kutoka juu, masharti mengine ni kutoka chini kwamba uwe na vyama huru vya wafanyakazi ili hawa mabepari wa ndani wasitumie kisingizio cha uwekezaji kuwanyonya wafanyakazi kupita kiasi, wanakuwa wanadhibitiwa na vyama vya wafanyakazi. Haya ndiyo masharti, ninavyoona mimi, kama umedhamiria kujenga uchumi wa kitaifa.

Ulipaji wa kodi
Suala la kodi ni muhimu, kwa serikali kukusanya mapato yake na mapato haya yakatumika kutoa huduma kwa jamii, huwezi ukajenga uchumi imara kama huna watu wenye afya imara, wenye elimu, huwezi. Kulikuwa na wakati sekta kama elimu, afya na maji zilichukuliwa kama sekta za huduma siyo za uzalishaji lakini sasa dhana imebadilika kabisa, dhana ya kimaendeleo ni kwamba elimu, afya, maji safi hizo siyo sekta za huduma ni sekta za uzalishaji kwa sababu wazalishaji ni nani, ni wananchi wenyewe, sasa kama hukuwekeza katika wazalishaji hao huwezi ukaendeleza uchumi wako.
Kwa hiyo dhana ni tofauti kabisa sasa, unapowekeza kwenye elimu, kwenye afya na hili ni jukumu la serikali siyo mambo ya kuachia soko huria, huwezi ukaachia soko huria, kwa kuwa unawekeza kwenye uchumi wako, unafanya uchumi wako uwe endelevu, na katika hili unahitaji mapato.
Swali linakuja baada ya kukusanya kodi una mpango gani wa kutumia hiyo kodi, na kuhakikisha kwamba watendaji wako wanawajibika kutoa zile huduma kwa wananchi hasa wa chini. Lakini hili huwezi ukasema katika siku hamsini, lakini kuna dalili unaziona hapa na pale. Kuyafanya mambo haya lazima ujenge mfumo uwe na dira unakoelekea, hufanyi uamuzi ambao ungongana, uamuzi wowote unalenga kujenga uchumi wa kitaifa hata pale unapowekeza katika huduma, dhamira iwe ni kuwekeza kwenye hali za watu wako ili uweze kujenga uchumi.
Miiko ya uongozi na maadili
Hakuna mtu anazaliwa na maadili, mara nyingi tunawapotosha watu kwa kweli, maadili yanatokana na mfumo uliopo. Wakati wa Mwalimu tulikuwa na miiko ya uongozi. Miiko ile haikubuniwa tu, ilikuwa na mizizi katika mfumo wenyewe. Wewe kiongozi unaongoza ujenzi wa nchi ya kijamaa huwezi ukahubiri ujamaa wakati wewe siyo mjamaa, wakati wewe unapora mali ya wananchi huwezi ukawa mjamaa.
Kwa hiyo chagua kama unataka kuwa kiongozi wa jamii inayotaka kujenga ujamaa lazima utii miiko hii kama hutaki sawa uko huru, ndiyo ilikuwa maana ya miiko, halikuwa suala la maadili ulikuwa unabanwa kuchagua sifa zilizopo. Sasa leo hatuna miiko tunazungumza maadili, yatatoka wapi? Wewe kama kiongozi wa serikali katika mfumo tulionao, wa kibepari, tena ubepari wenyewe siyo imara, ubepari uchwara wewe utafundisha nini watoto wako, utawaambia wasitafute biashara, wasichume faida, yule mtoto atakusikia? Hawezi kwa sababu mfumo wenyewe ni tofauti na katika siku hamsini huwezi kuyaona haya.
Ikiwa kweli amedhamiria itambidi huko mbele ya safari awaambie viongozi wake kuchagua moja, na tusijiingize, kwa maoni yangu inawezekana nimekosea, lakini tusijiingize kwenye mjadala wa mgongano wa maslahi, wewe umekuwa waziri ulikuwa na biashara yako unaweza kuendelea na biashara yako lakini uweke kwenye trust (bodi ya wadhamini) hapana chagua moja ama uwe mfanyabiashara au uwe kiongozi.
Uchumi wa Bandari
Kuna mambo mawili ningeweza kusema moja ni kuhusu Bandari, kwa kweli tumejaliwa nafasi ya kijiografia nzuri sana, tumezingirwa na nchi kama nane hivi, tungeweza kutumia bandari yetu kukusanya na kulimbikiza mtaji mkubwa sana. Tungekuwa tunapata mapato makubwa sana na tungeweza kutumia mapato hayo kuwekeza na kuendeleza sekta zingine, bahati mbaya mapato yote ya bandari yamepotelea mifukoni mwa watu.
Hatujaweza kutumia bandari yetu vizuri, leo tuna tatizo la usafiri nchini, sawa tunajenga barabara, lakini nchi kubwa kama Tanzania haiwezi kutegemea barabara, kipaumbele kilikuwa ni kujenga njia za reli, ndiyo ingekuwa hasa njia zetu za usafiri na maji. Lakini hata ile reli tuliyorithi tumeharibu, Reli ya Tazara tumeharibu.
Kuhusu suala la Bunge kama linatimiza wajibu wake, ningesema dhati kabisa kwamba katika mfumo wa vyama vingi tulio nao hakuna hata chama kimoja ambacho kina program, dira ya hayo niliyozungumza. Ni kwa mara ya kwanza kabisa baada ya miaka 30 tunampata kiongozi ambaye angalau anaonyesha mwelekeo wa kujenga aina ya uchumi anaotaka. Hebu nieleze katika miaka hii 30 umemsikia nani akizungumzia mwelekeo wake kuhusu aina ya uchumi anaotaka kujenga, aina ya nchi ambayo anataka kujenga, nani? Watu wanatumia neno mfumo siku hizi, lakini mfumo wanaozungumza haueleweki, kwangu mimi ukisema mfumo maana yake ni mfumo wa uzalishaji, mfumo wa uchumi ndiyo hasa kitovu cha kila kitu tunataka mfumo wa uzalishaji uwe wa namna gani, lazima uainishe hilo. Ndiyo maana nimesema kwamba kuweza kuangalia hizi kashfa hapa na pale, sawa, lakini hatimaye lazima ujiulize swali, hii kashfa inatokana na nini? Chanzo chake ni kipi? Kwa nini mtu anaweza kufanya mambo kama yale, nini kinamruhusu? Ni kwa sababu ana uhuru wa kujilimbikizia, kwa hiyo unatumia cheo chako kama nafasi ya kujilimbikizia mtaji.
Magufuli kama Sokoine
Kuna mambo yanafanywa na Rais Magufuli ambayo yanaelekea-elekea kama ya Sokoine (Edward Moringe, Waziri Mkuu wa zamani), lakini kuna haja mimi naona kwa upande wake kuangalia mambo kwa undani zaidi, nafikiri yeye mwenyewe anajua kwamba siyo rahisi kukabiliana na mfumo tulionao ambao umejengeka. Kwa sababu makundi na matabaka ambayo yanafaidika na mfumo huu wanakuwa na njia zao za kuhujumu na mara nyingi sana hawakuhujumu wazi wazi au kwa vitendo vinavyojulikana, hawa ni hatari zaidi, wanafanya chini chini wengine wanafanya kwa jazba kuonyesha kwamba wewe ni zaidi kuliko yule, katika hili unadhalilisha kiongozi wako na hii ni njia mojawapo ya kuhujumu mtu ili ionekana ni upuuzi tu huo, yule anajipendekeza kwa kufanya ya kukuiga lakini kwenda mbali zaidi.
Mafunzo kutoka kwa Sankara
Thomas Sankara alikuwa ni kijana aliyekuwa na dhamira na mwelekeo, na alikuwa anaelewa anachotaka kufanya. Lakini kama kuna kitu cha kujifunza kutoka kwa Thomas Sankara, aliuawa na nani, mwenzake mwenyewe waliofanya mapinduzi pamoja, wale waliomuunga mkono wakati wa mapinduzi hawakutaka kwenda mbali kiasi cha yeye alivyotaka, wakamuuwa. Ndiyo maana kila wakati ninasema siyo kwamba hatuna viongozi katika Afrika, lakini viongozi kama hawa lazima waelewe kitu kimoja, wawe na imani kubwa na watu wao, wajikite kwa watu wao, wawashirikishe watu wao, wasitegemee tu viongozi wenzao au mfumo. Ndiyo maana nimesema yale aliyofanya pale mwanzoni tu yalikuwa na umuhimu wake, wananchi wakiwa upande wako, siyo kwa kushangilia tu, lakini pia kushirikishwa wao watakulinda.
Kwa ujumla kuna dalili za kuwa na matumaini, hatuwezi kuwa na uhakika lakini dalili zipo, sasa tuangalie zinaenda wapi …mwelekeo wake, viongozi anaochagua, namna wanavyotatua matatizo mbalimbali, lakini mimi binafsi ningependa kusema kwamba aweke imani kwa wananchi wake na pili awashirikishe, kwa hiyo, aangalie suala la demokrasia kwa jicho la kuwashirikisha wananchi. Wananchi waambiwe, wahamasihwe tuwe pamoja tunataka kujenga nchi ambayo itajali watu wa hali ya chini na wao washirikishwe.
Tuanze kufikiria muundo wa demokrasia ya wananchi moja kwa moja, na bahati nzuri tunao, kwa mfano leo vijijini tuna mkutano mkuu wa kijiji, tuna serikali za vijiji na kwangu mimi kijiji ndiyo kitovu cha demokrasia, tusifikirie tu mambo ya uchaguzi na Bunge tufikirie vijiji.