Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, inatarajia kupanga tarehe ya usikilizwaji wa kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi Jimbo la Mbagala, Februari 4, mwakani.

Jaji Wilfred Dyansobera alitoa kauli hiyo jana baada ya upande wa mdai kuomba kufanya marekebisho madogo kwenye hati ya madai.

Kesi hiyo ilifunguliwa na aliyekuwa mgombea wa ubunge CUF, Kondo Bungo akipinga matokeo yaliyompa ushindi, Issa Mangungu wa CCM.

Wadaiwa wengine katika kesi hiyo namba 1 ya mwaka 2015, ni msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo hilo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Jana wakati kesi hiyo ikitajwa kwa mara ya kwanza, Wakili wa mdai, Juma Nassoro aliiomba mahakama hiyo ifanye marekebisho madogo ya sheria kwenye hati ya madai.

Mahakama ilikubaliana na ombi hilo baada ya Wakili wa mdaiwa wa kwanza (Mangungu), Samson Mbamba kuileza mahakama kuwa hana pingamizi nalo.