Chama cha Wananachi (CUF) , kimewataka Wazanzibari kusubiri taarifa rasmi itakayotolewa na viongozi wanaoshiriki mazungumzo ya kutafutia ufumbuzi wa mgogoro wa Zanzibar badala ya kusikiliza kauli zinazotolewa na upande mmoja.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma wa CUF, Ismail Jussa alisema kauli rasmi itatolewa baada ya kumalizika kwa vikao vya wakuu hao na uamuzi wake kutangazwa. Aliwataka Wazanzibari kuvuta subira na kumpa nafasi Rais John Magufuli ambaye anaendelea na juhudi katika ngazi za juu kabisa za kuhimiza kupatikana ufumbuzi wa haraka wa mgogoro huo.

Kauli ya CUF imefuatia taarifa iliyotolewa na CCM siku nne zilizopita baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati Maalumu ya chama hicho iliyowataka wanachama wao kujitayarisha na uchaguzi wa marejeo.

“Wazanzibari wapuuze taarifa ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar, kwani haina lolote jipya zaidi ya kutaka kufunika kombe,” alisema Jussa.