Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu wa Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Severine Niwemugizi amesema hotuba ya Rais Magufuli ni nzito inayohitaji kuungwa mkono na watendaji wote wa Serikali kuanzia ngazi ya chini hadi Taifa.Kauli ya kiongozi huyo inatokana na Rais Magufuli kuwahakikishia Watanzania kuwa atapambana kufa na kupona dhidi ya vigogo ambao wamekuwa wakihujumu maendeleo ya umma kutokana na rushwa, ufisadi na uzembe.Alisema kutokana na nchi ilipofikia, Watanzania wanapaswa kumuunga mkono katika mkakati wake wa kupambana na ufisadi.Askofu* huyo alitoa kauli hiyo jana kwenye ibada maalumu iliyofanyika kwenye Parokia ya Chato, kwa lengo la kumwombea Rais Magufuli ili aweze kutimiza majukumu yake katika kuwaletea maendeleo Watanzania.“Hotuba ya mheshimiwa Rais Magufuli ilinifurahisha sana... lakini iliitia woga sana kwa sababu ya wale viongozi wanaoona wamemuingiza madarakani mwenye kuziba mianya ya rushwa, hivyo watajitahidi sana kuhujumu afya yake na hata malengo yake kwa kuwa amejiita ni mtumbua jipu.“Mtakumbuka kabla ya kuhitimisha hotuba yake aliwaomba Watanzania tumwombee, ndiyo maana sisi kama kanisa tumeamua kumwombea ili Mungu amtangulie katika mambo yote... tunatambua atakutana na vigingi vya kila aina.”Mbali na kumwombea kutimiza wajibu wake, ibada hiyo pia imetumika kuliombea Taifa kudumisha amani upendo na mshikamano kwa kuwa bila ya amani, nchi haitaweza kutawalika.“Tunatakiwa kutumia muda wetu mwingi kuliombea Taifa amani... Rais Magufuli atapata wakati mgumu sana kuiongoza nchi hii iwapo hapatakuwa na amani,” alisema.Akizungumza katika ibada hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Chato, Shaaban Ntarambe alisema kwa sasa Watanzania wanatakiwa kuwa wamoja kwa kumuunga mkono Rais aliyeko madarakani ili aweze kutimiza majukumu yake.Alisema ili wananchi waweze kufikia maendeleo ya kweli, wanapaswa kufanya kazi kwa bidii kutimiza falsafa ya “hapa kazi tu” hatua itakayowasaidia kuinua uchumi wao.