HUKUMU ya kesi inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Shekhe Ponda Issa Ponda, imeshindwa kutolewa jana kutokana na Hakimu Mwandamizi wa Mahakama ya Mkoa wa Morogoro, Mary Moyo kuwa mkoani Dodoma kwa shughuli za kikazi.

Hakimu Erick Rwehumbiza aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 30, mwaka huu. Alisema Hakimu Moyo ambaye ndiye anaisikiliza hadi hatua ya kuandika hukumu, kuanzia Novemba 16, mwaka huu yuko mkoani Dodoma kwa ajili ya kuhudhuria mafunzo maalumu ya kushughulikia kesi za uchaguzi na anatarajiwa kurudi kutoa hukumu hiyo Novemba 30.

Aliamuru Shehe Ponda aliyeletwa mahakamani hapo kwa ajili ya hukumu arudishwe rumande. Upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Juma Nassoro na upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili wa serikali mwandamizi Bernard Kongola, ulieleza kuwa wameshakamilisha hatua zote kesi na kwamba wanachosubiri ni hukumu hiyo.

Nassoro akiwa nje ya mahakama aliwaambia ndugu, jamaa na wafuasi wa Ponda waendelee kuwa watulivu na wavumilivu kwa vile suala lililobakia ni la Hakimu kutoa hukumu Novemba 30 mwaka huu.

Alisema, wao wakiwa mawakili wa utetezi kesi hiyo wamemaliza sehemu yao na iliyobakia ni kwa hakimu kuamua siku ya kutoa hukumu na kwamba wote wanasubiri hukumu hiyo.

Baada ya kuahirishwa kwa hukumu hiyo, wafuasi hao waliamua kutawanyika kutoka katika eneo la mahakama hiyo na kuelekea msikiti wa Ijumaa. Shehe Ponda alifunguliwa kesi namba 128/2013 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani hapa.

Awali alikuwa akikabiliwa na mashtaka matatu anayodaiwa kuyatenda Agosti 10, mwaka 2013 katika eneo la Kiwanja cha Ndege Manispaa ya Morogoro. Alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Agosti 19 mwaka 2013 kwa mashitaka hayo matatu na baadaye alifutiwa shitaka moja na kubakia mawili ambayo ni kutoa maneno yenye kuumiza imani za dini na kushawishi watu kutenda kosa.