Wapendwa viongozi wetu mbalimbali wakiwemo wa CCM, Maaskofu hasa Mwadhama wameibuka na kauli kwamba tuachwe tuisome tuielewe halafu ndio tuipigie kura baada ya kuielewa.
Kwa unyenyekevu mkubwa ningeshukuru viongozi wetu hawa wapendwa sana watupatie fomula ya kutuwezesha kuisoma na kuielewa ili tuweze kuipigia kura.
Kama BMK ilitumia zaidi ya siku 130 kuitunga nakumbuka siku 60 walizotoa hazikutosha wakaongezewa 70 ndipo wakakamilisha tena ilikuwa bahati kwamba walibaki watu wa chama na mlengo mmoja tu. Itakuwaje kwa nakala milioni 2 Tanzania nzima kuisoma kuielewa na kuipigia kura ya ndiyo ama hapana?
Pengine ijulikane kwamba Viongozi hasa wa kiroho wanatumia falsafa na diplomasia ya unyenyekevu tu maana wanajua kwa hakika kwamba haitawezekana kuipata nakala ya Katiba pendekezwa na tukaisoma na kuielewa na tuipigie kura stahiki.
Jukwaa la Wakristo Tanzania ambalo limesheheni wataalamu mbalimbali wakiwemo wanasheria na wahadhiri wa sheria wa vyuo vikuu tayari washafanya kazi ya uchambuzi na kuweka msimamo wao hadharani. Sasa kwa nini tena serikali na baadhi ya viongozi wa madhehebu ya dini wageuke na kuwapinga Jukwaa la Wakristo Tanzania kwa kutoa maoni yao?
Mbona suala la maoni liko wazi kwa mujibu wa Katiba iliyopo sasa? Hata wakati wa ufunguzi wa Bunge Maalum la Katiba Kiongozi wetu Mkuu naye alipata nafasi akatoa maoni yake baada ya Mzee wa Viwango kubadili Kanuni za Bunge hilo nani aanze katika ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na Rais wa Jamhuri ya Muungano?
Ili tuweze kuelewa sawasawa Tunawaomba viongozi wa serikali yetu Sikivu watufungulie Tovuti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ili tufanye ulinganishi wa maoni tuliyotoa kwenye Tume na hicho kilichomno kwenye Katiba Pendekezwa. Kama Tovuti ta Tume haitafunguliwa ni wazi mpango wetu wa kupigigiwa kura ya Ndiyo Katiba yenu utakwama mapema asubuhi na mapema.
Connect With Us