KAMPUNI ya Lamudi Tanzania imezindua namba maalum itakayotoa fulsa kwa wanunuzi, madalali na wamiliki wa viwanja, nyumba na vitu visivyohamishiwa kufanya biashara kupitia simu zao za mkononi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Lamudi Tanzania, Mustafa Suleimanji ameliambia MwanaHALISI Online, kuwa namba itakayotumika 0800710022 na itakuwa bure kwa anayehitaji.

Suleimanji alisema Watanzania wengi kwa sasa wanamiliki simu za mikononi huku wakitumia mitandao, lakini wameshindwa kuzitumia kwa kununua nyumba, kupanga, kununua viwanja na mali zisizohamishika.

Alisema kutokana na kutojua matumizi ya mtandao kupitia simu zao za mkononi Watanzania wengi wamekuwa wakitumia muda wao mwingi kuzunguka kutafuta nyumba za kupanga au kununua, lakini sasa Lamudi imejipanga kumaliza tatizo hilo.

“Kwa kutumia simu yako mkononi unaweza kufanya manunuzi ya mali zisizohamishika ukiwa nyumbani bila ya kupoteza muda. Unapopiga namba hiyo utapata maelekezo jinsi ya kupata mahitaji yako kwa kutumia simu yako,” anasema Suleimanji.

Suleimanji anaongeza kuwa kwa kupitia namba hiyo mteja ataweza kuunganishwa na madalali pamoja na wamiliki wa mali hizo, bila ya kupoteza muda.

Mkurugenzi aliongeza kuwa lengo la Lamudi ni kufanya maisha ya kila Mtanzania kuwa rahisi na kwenda sambamba na tekinolojia ya ulimwengu wa sasa.