Close

Results 1 to 6 of 6
Like Tree1Likes
 • 1 Post By MV Salama

Thread: ELIMU YA MAHUSIANO, KARIBU.

 1. #1
  Senior Member MV Salama's Avatar
  Join Date
  Jan 2014
  Location
  New York
  Posts
  1,880
  Rep Power
  8
  Likes Received
  104
  Likes Given
  80

  ELIMU YA MAHUSIANO, KARIBU.

  MWANAUME NI NANI KATIKA JAMII?

  o Mwanaume ni kiongozi wa familia
  o Mwanaume ni mlinzi wa mwanamke pamoja na familia
  o Mwanaume ni mfano wa kuigwa na jamii
  o Mwanaume ni mrithi wa Mungu

  MWANAUME MWENYE ASILI YA MUNGU (MWENYE MAADILI MAZURI)

  o Ni mnyenyekevu wakati wote
  o Ni mvumilivu wakati wote
  o Yupo tayari kusuluhisha kesi yake na kuanza upya
  o Ni mwepesi kusamehe na kusahau
  o Ni mtu mwenye utu na anathamini utu wa mtu
  o Anajali watoto na mke wake pia
  o Hatakama atakuwa si muaminifu hujitahidi sana mke wake asijue

  MWANAUME MWENYE ASILI YA DUNIA (ASIYE NA MAADILI MAZURI)

  o Ni mkorofi kupindukia
  o Hana utu wala kujali
  o Ni mtu wa lawama wakati wote
  o Hana hofu kwa chochote anachokifanya
  o Huhesabu makosa wakati wote
  o Hana maneno ya faraja kila wakati hulaani tu
  o Hana moyo wa kusamehe, siyo rahisi kesi yake imalizike kwa amani

  v Kundi la kwanza linamtambulisha mwanaume mwenye anayefuata muongozo mzuri wa malezi kutoka kwa wazazi wake na pia sheria za dini ambazo zinamuandaa kuwa mwanaume mwenye majukumu ya mke na familia. Hivyo anapokutana na mwanamke asiye na maadili inamuwia vigumu sana kumbadilisha tabia na kama Mungu asipoingilia kati mahusiano haya kunaweza kumfanya mwanaume huyu asitamani tena kuoa au kuwa katika mahusiano maana huwaza kupenda na endapo atapata mwanamke mwenye maadili ndoa yao itakuwa nzuri sana kutokana na asili yao.

  v Kundi la pili linamtambulisha mwanaume asiye na malezi na asiye jua nini wajibu wake kama mwanaume. Mwanaume huyu anakuwa katika hali kama hii endapo kwa upande mmoja wazazi wake walichangia katika malezi mabovu au wazazi walijitahidi sana kumfundisha lakini hakufundishika, Mwanaume huyu anapokutana na mwanamke mwenye maadili au aliyefundishwa vizuri tangu mwanzo kuwa ipo siku moja atakuwa mke wa mtu itamuwia vigumu mke huyu kuchukuliana na huyu mwanaume na atahangaika sana kutaka kumbalisha lakini haitawezekana kwa kipindi kifupi tu. Itamlazimu kulipa gharama ya muda mrefu na kumtafuta Mungu zaidi kuliko kutumia akili zake mwenyewe.

  v Katika makundi yote haya tunaweza kuona mwanaume uliyenae wewe yupo katika kundi gani na asili gani ili unapoanza kushugulika na kasoro unazoziona katika ndoa au mahusiano yako utambue mwanaume huyo asili yake ni nini na jinsi gani utaweza kusaidiana naye katika safari hii ya mahusiano au ndoa yenu.


  MWANAMKE NI NANI KATIKA JAMII?

  o Mwanamke ni msaidizi wa mwanaume
  o Mwanamke ni taji ya mwanaume
  o Mwanamke ni mjenzi wa mji wake na nyumba yake
  o Mwanamke ni kipenzi cha watoto na mume
  o Mwanamke ni mwalimu wa familia
  o Mwanamke ni mshawishi wa tabia njema kwa jamii inayomzunguka

  MWANAMKE MWENYE ASILI YA MUNGU (MWANAMKE MWENYE MAADILI)

  o Hana haraka ya mambo
  o Mvumilivu, mnyenyekevu, mtiifu, mkweli, anaheshima, anajituma, ana utu
  o Yupo tayari kufanya suluhu na kusahau
  o Yupo tayari kujifunza kutokana na makosa
  o Ana mapenzi ya dhati nay a ukweli
  o Anajali watoto na mume wake pia pamoja na jamii yote inayomzunguka
  o Hayupo tayari kumsaliti mume wake hata kama sababu zote anazo.

  MWANAMKE MWENYE ASILI YA DUNIA (ASIYE NA MAADILI)

  o Ni mkorofi
  o Hasira zake huwa karibu na za wazi wazi sana
  o Kinywa chake hutoa matusi na lawama wakati wote
  o Hukusanya makosa ya mume wake wakati wote
  o Huwa na upendo wa mtego, hana upendo wa dhati
  o Hupenda kupokea zaidi ya kutoa
  o Hulazimisha mambo yafanyike hata kama haiwezekani kwa wakati huo.

  v Katika kundi la kwanza tunamuona mwanamke mwenye asili ya mungu ambaye hutambulika kama mwanamke shujaa mwenye maadili ya kuwa mke mwema na aliye andaliwa vizuri kuwa mke bora kwa mume na familia nzima, Mwanamke huyu anapokutana na mwanaume mwenye asili ya dunia hujuta sana kwanini ameingia katika mahusiano na mtu huyu, inamuwia vigumu kuikabili tabia ya mwanaume huyu na kuona wanaume wote ni maadui na kama ikishindikana kupata msaada wa kumtoa katika eneo hilo basi hujikuta akibaki mnyonge na mwenye kilio wakati wote hatimae kutokuwa katika mahusiano tena. Anapobahatika kukutana na mwanaume ambaye ana maadili mahusiano yao huwa ya amani sana na hata ndoa yao huwa inadumu kwa kiasi kikubwa sana.

  v Kundi la pili linamtambulisha mwanamke asiye na malezi na asiye jua nini wajibu wake kama mwanamke. Mwanamke huyu anakuwa katika hali kama hii endapo kwa upande mmoja wazazi wake walichangia katika malezi mabovu au wazazi walijitahidi sana kumfundisha lakini hakufundishika, Mwanamke huyu anapokutana na mwanaume mwenye maadili au aliyefundishwa vizuri tangu mwanzo kuwa ipo siku moja atakuwa mume wa mtu itamuwia vigumu mume huyu kuchukuliana na huyu mwanamke na atahangaika sana kutaka kumbalisha lakini haitawezekana kwa kipindi kifupi tu. Itamlazimu kulipa gharama ya muda mrefu na kumtafuta Mungu zaidi kuliko kutumia akili zake mwenyewe.

  v Katika makundi yote haya tunaweza kuona mwanaume uliyenae wewe yupo katika kundi gani na asili gani ili unapoanza kushugulika na kasoro unazoziona katika ndoa au mahusiano yako utambue mwanaume huyo asili yake ni nini na jinsi gani utaweza kusaidiana naye katika safari hii ya mahusiano au ndoa yenu.

  MAPENZI NI NINI?

  Kutokana na tafsiri mbali mbali na mijadala mbali mbali inaonesha mapenzi ni ‘’ mkusanyiko wa hisia za binadamu zinazopelekea kujenga urafiki wa kudumu kati ya mwanamke na mwanaume au mtu na mtu mwingine.’’

  MPENZI NI NANI?

  o Ni binadamu aliyejitoa kwa ajili yako, kusaidiana na wewe katika shida na raha
  o Ni mtu yeyote aliyetayari kuumizwa kwa ajili yako
  o Ni binadamu aliye tayari kushauriana na wewe pale anapoona umekosea
  o Ni binadamu aliyetayari kuona unafanikiwa badala ya kuangauka
  o Ni binadamu aliyetayari kushirikisha hisia zake za kimapenzi na wewe bila kificho

  KUFANYA MAPENZI NI NINI?

  o Kuonesha hisia zako za kimapenzi kwa vitendo
  o Kufanya vitendo vya upendo kwa wale wote walio shirikiana na wewe ktika shida au raha
  o Kujitoa kwa jamii nzima zaidi ya kusubiri kupokea zaidi

  KUSUDI LA KUFANYA MAPENZI NI NINI?

  o Kumfurahisha mpenzi wako
  o Kufurahisha mwili wako na nafsi yako
  o Kupata watoto/ kuanzisha familia kwa kupata watoto
  o Kujenga ushirikiano wa kudumu baina yako na mwenzi wako/ jamii inayokuzunguka
  o Kuonesha hisia za mapenzi kwa vitendo na kufanya suluhu ya matatizo yenu.

  MAPENZI YANABEBWA NA VITU VIWILI VIKUBWA AMBAVYO NI:
  UPENDO NA HISIA ZA MAPENZI.

  UPENDO NI NINI?

  v Ni tendo la hiari kutoka moyoni mwa mtu analo kusudia kulifanya kupitia vitendo vya ukarimu, upendo siyo kujivuna, siyo kujisikia wewe ni bora kuliko wengine, siyo kulipiza kisasi, siyo kulaani bali kubariki n.k

  v Upendo ni kusaidiana katika raha na shida pia kutoa shukurani kwa Mungu na jamii nzima pale unapokuwa umeshirikiana nao katika jambo lako lolote.

  v Upendo husaidia kumaliza ugomvi na kufanya jamii nzima iwe na amani

  v Upendo mara nyingi unapokuwa ni wa dhati hauwezi kupotea kamwe kwani kila sku vitendo vya upendo husaidia kuongeza ladha ya mahusiano. Hivyo unapoona vitendo vya upendo vinapungua katika nyumba yako ujue ni rahisi kupoteza amani iliyomo humo ndani.

  v JUKUMU LAKO KAMA MWANAUME AU MWANAMKE ULIYE KATIKA MAHUSIANO NI KUPENDA KWA DHATI ILI KUFANYA VITENDO VYA UPENDO VIZAE AMANI KATIKA NYUMBA YENU NA MAHUSIANO YENU.

  HISIA ZA MAPENZI NI NINI?

  o Hapa kila mmoja wetu atakuwa na jibu lake kuhusu swali hili lakini hebu na tuziangalie hisia za penzi ni nini maana yake.

  o Hisia za mapenzi ni ile hali isyo kifani, msisimko, shauku, kujiskia raha mara zote unapoona mwenzi wako anarudi kutoka katika shughuli za kila siku, au anarudi kutoka safari, au anapokuwa karibu na wewe.

  o Hisia za mapenzi ni tendo linalonesha mapenzi ya dhati kati ya wewe na mpenzi wako jinsi mlivyoshibana.

  o Hisia za mapenzi ni nzuri kupindukia ndo maana mamilioni ya wasanii wa muziki duniani kote wamekuwa wakiimba nyimbo zinazolenga mapenzi na wapenzi.

  o Wengi wetu tumeshapatwa na hisia za mapenzi kali sana kiasi kwamba tumebaki tukijilaumu na kufikia hatua ya kujiua au kuwaua wale wanaoingilia mapenzi yetu. Hisia za mapenzi zaweza kujenga undugu wa kudumu na waliokaribu yako au kubomoa/kuvunja undugu na waliokaribu yako.

  UKWELI KUHUSU HISIA ZA MAPENZI UPOJE?
  o Hisia za mapenzi hujengwa na vitendo vya upendo
  o Hisia za mapenzi huweza kutoweka na kuhamia mahali popote pale penye upenyo ambapo vitendo vya upendo hupatikana kwa urahisi.
  o Hisia za mapenzi huweza kurudisha mapenzi yaliyoharibiwa vibaya kwa kupata vitendo vya upendo wa dhati mara dufu ya ilivyokuwa mwanzo.
  v Tatizo ulilonalo leo katika NDOA yako au mahusiano yako ni vyema ukalifanyia uchunguzi mapema ili kujuwa kama limetokana na kushuka kwa kiwango cha UPENDO hivyo kupelekea HISIA ZA MAPENZI kupotea na kuvunja amani yako na mpenzi wako.

  · FANYA TATHIMINI YA MAHUSIANO YAKO, NA UJIHOJI MASWALI YAFUATAYO!
  (i) Unauhakika kuwa unafahamu hisia za mapenzi, na unajuwa zinachochewa na vitedo vya upendo?
  (ii) Unafahamu gharama ya kupoteza vitendo vya upendo?
  (iii) Upo tayari kupoteza NDOA/MAHUSIANO kutokana na kutokuwa mtafiti wa mbinu mbali mbali za kudumisha mahusiano au ndoa yako?
  (iv) Ulishawahi kumpenda mume / mke wako kwa vitendo?
  (v) Unatarajia nini kutoka kwa mume/ mke wako unapofanya vitendo vya upendo? (b) Unatarajia kupokea zaidi au kutoa zaidi?
  (vi) Wewe ni muaminifu kwa kila jambo katika mahusiano uliyopo? (b) Unauwezo gani wa kusimamia uaminifu wako na mwenzi wako linapokuja tatizo la KUKOSA UAMINIFU?
  (vii) Upo tayari kusamehe na kusahau? (b) Je upo tayari kucheza vizuri katika nafasi yako?
  (viii) Upo tayari kupanga mambo yako upya? (b) Upo tayari kuangalia mazuri ya mwenzako na kukumbuka mazuri aliyokutendea kuliko kuangalia mabaya na makosa madogo madogo anayokosea eidha kwa kujuwa au kutokujuwa kama kwako ni makosa?

  MAMBO YA KUANGALIA NA KUZINGATIA KATIKA SWALA LA MAPENZI!
  (i) Kumbuka kuwa penzi ni kitendo, kitendo cha kumjali na kumfikiria mwenzi wako na kuwa mpole, muungwana, mwenye subira, na kuelewa kuwa huyo mpenzi wako ana uhuru wa kuweza kuchagua kukupenda au kutokukupenda milele bila kuangalia hasara zitakazopatikana.
  (ii) Kumbuka kuwa hisia za penzi ni hisia tu, zinaweza kuja kwa wingi au zinaweza kutoweka kabisa.
  (iii) Endapo utaona hisia za penzi zimeanza kutoweka unaweza kufanya jitihada kuzirudisha kwa kufanya matendo ya upendo bila kujali faida au hasara zitakazotokea, unachohitaji hapa ni kurudisha penzi lako katika mstari ulionyooka!
  v Ili kudumisha NDOA yenu au mahusiano yenu itakutegemea wewe kama wewe eidha ni mwanamke / mwanaume. Kwa upande wa mwanamke ana paswa kuonesha upendo zaidi kuliko kupokea, isipokuwa pale ambapo mwanaume ameshindwa kabisa kupokea upendo wako.

 2. #2
  Senior Member MV Salama's Avatar
  Join Date
  Jan 2014
  Location
  New York
  Posts
  1,880
  Rep Power
  8
  Likes Received
  104
  Likes Given
  80

  Re: ELIMU YA MAHUSIANO, KARIBU.

  KILA ndoa ina matatizo, na yanaweza kufumuka wakati wowote. La muhimu ni kwamba unapokuwa umeamua kujiingiza katika maisha ya ndoa unapaswa kujifunza jinsi ya kukabiliana na matatizo hayo ili yaweze kuisha salama na ndoa kuendelea kuwa salama.

  Bila kujali umeenda umbali gani katika barabara hii ya ndoa, zipo kanuni rahisi lakini za muhimu za usalama katika barabara hii. Si rahisi sana kuzitekeleza kanuni hizi, kwa wanandoa walio wengi, lakini ni lazima kuzitekeleza iwapo wahusika wanapenda ndoa yao iwe salama.

  Iwapo utazingatia kanuni hizi, utaifanya ndoa yako kuwa imara zaidi. Katika usalama huu utapata pia marupurupu – furaha, ngono, kuaminiana (kuaminiwa), mapenzi moto moto na kadhalika. Hebu sasa na tuziangalie kanuni zenyewe: -

  1. ONESHA MATENDO YA KIMAHABA

  Usipojishughulisha kwa lolote lile kwa ajili ya kumfurahisha mpenzi wako utasababisha mwenzako achoke na hata kufikia mahala akakasirika. Ili kuepuka haya, hakikisha kuwa unayapa kipaumbele mambo ambayo yanamfanya mpenzi wako kujihisi maalumu kwako. Na njia rahisi zaidi ni kuwekeza katika matendo madogo madogo ya kimahaba.

  Kumbuka, kauli moja hasi au ya kuvunja moyo inaweza kuhitaji kauli kama ishirini chanya ili iweze kufifia (si kufutika) akilini mwa mpenzi wako. Hii ina maana kwamba, badala ya kumlaumu mpenzi wako, wekeza zaidi katika kumsifia katika mambo yake, au mambo anayoyafanya utakavyo.

  Msifie mpenzi wako kwa nguo yake mpya, msifie kwa kukujali, mpigie simu ofisini kwake na kumwambia kuwa ulikuwa unamuwaza na kadhalika. Isipokuwa, hakikisha kuwa sifa hizi na kauli hizi za mahaba zinadhihirika kutoka moyoni, zisije kuwa kama mazoea tu.

  Iwapo utafanya hivi, ni rahisi sana kumfurahisha mpenzi au mwenzi mwenye nia njema na wewe. Kumbuka mambo yenu yalianza hivi hivi, pale mlipokuwa bado mnafukuziana. Matendo madogo ya kimahaba hayapaswi kuwa na mwisho, maana ndiyo hudumisha msisimko wa wenza.

  2. TUMIA HISIA ZA MGUSO

  Hisia za mguso ni muhimu sana kwa wapenzi. Na njia mojawapo ya kumweka mpenzi wako katika utayari wa kukupa kila kitu ni kumshika mkono unapotembea naye kwenda dukani. Naam, Afrika hii unaweza kusemwa na hata kuchekwa, lakini la muhimu kwako ni kwamba unamfanyia mwenzi wako wa maisha.

  Unapomsalimia mwenzi wako, gusa mashavu yake kwa ncha za vidole vyako. Jikumbushe jinsi ulivyokuwa unamgusa katika siku za kwanza, kabla hujamzoea. Ulikuwa ukimgusa kwa huba na tamaa kubwa. Mbusu kila panapoweza kubusika, pitisha mkono wako kwenye nywele zake, na kadhalika. Kugusa ni lugha muhimu ya mapenzi. Itaongeza msamiati wako wa mapenzi.

  Sanjari na kumgusa, onesha pia kuwa unamuunga mkono mwenzako. Unapotokea ugomvi, wewe nenda upande wa mwenzi wako. Pia mtunzie siri zake maana wewe ndiwe mwandani wake. Hata kama huko kazini au kokote watu watazungumza siri za wenzi wao, wewe siri za mwenzako ziache kuwa baina yake na wewe.

  3. KUMBUKA HAKUNA MKAMILIFU

  Unapokasirika, au kukatishwa tamaa, au kuvunjwa moyo au kufadhaishwa, unaweza kushindwa kujizuia kumlaumu aliyekusababishia hali hiyo, hata kama mtu mwenyewe ni mwenzi wako wa maisha. Pia, ni kawaida kwa mtu kujaribu kumbadilisha mpenzi wake anapodhani ana udhaifu fulani.

  Hata hivyo, unapojaribu kumkosoa na kumrekebisha mpenzi au mwenzi wako unamweka katika hali ya kujitetea. Matokeo yake ni kwamba hatabadilika na pengine ataacha kuwajibika. Matokeo mengine ni kwamba furaha yake itaondoka. Kumbuka, unapomkosa mwenzako ni kama vile unapuuza asilimia 90 ya hulka yake njema ambayo ilikufanya uvutiwe kuwa naye.

  Kama kweli unataka kumpa kipaumbele mwenzako na kisha kutarajia mazuri kutoka kwake, basi badala ya kutaka kumbadilisha yeye, badilika wewe mwenyewe kwa kuondoa mapungufu yako mwenyewe. Iwapo utajirekebisha, mpenzi wako hatasubiri umlaumu au umgombeze, bali yeye pia atabadilika.

  Katika suala hili, ni vema kutambua kuwa hakuna mtu mkamilifu – si wewe, wala yeye, wala mwingine. Mungu tu ndiye mkamilifu. Siku nyingine mpenzi wako akifanya jambo ambalo unahisi linakukera, acha kuhemka. Badala yake, jifariji kwamba alikuwa na lengo zuri japo matokeo hayakuwa mazuri. Na kila siku, wiki au mwezi, chagua jambo moja ambalo unaliona kuwa zuri kwake, kisha litaje. Linaweza kuwa ucheshi, utani na kadhalika. Yaangalie hayo yaliyo chanya tu.

  4. FAHAMU KUGOMBANA VIZURI

  Migogoro katika ndoa ni kitu cha kawaida. Naam, wengine husema ndoa isiyo na migogoro ni sawa na kusema imekufa. La muhimu ni vile unavyokabiliana na migogoro hiyo.

  Kwa hakika, kushirikiana katika kutatua migogoro ni vema zaidi kuliko kuhangaika mwenyewe. Naam, kama kila mmoja atakuwa na nia njema, migogoro inaweza kuwa njia mojawapo ya kuzidi kushikamana na mwenzako. Ni kwa kufahamu namna njema ya kukabiliana na migogoro ndipo mtu huweza kumpenda mwenzake kama alivyo.

  Kumlaumu mwenzako ni kitu cha kuepuka kwa gharama yoyote. Pia, acha kukabiliana naye kwa maneno, kwani utakuwa unawasha moto ambao haitakuwa rahisi sana kuuzima. Wanandoa wenye furaha ni wale ambao huepuka sana kutumia vinywa vyao dhidi ya wenzao. Hawa hufahamu jinsi ya kuzuia mazungumzo kulipuka na kuwa ugomvi. Watu hawa hujitahidi kuepuka maneno ya kujiapiza kama “kamwe” na kadhalika.

  Iwapo ugomvi utatokea (naam, hakika utatokea), jaribu kubadilisha mada, ingiza ucheshi, mwoneshe mwenzako mapenzi ya ziada. Kama utabaini kuwa tayari umechelewa, tafuta suluhu kwa kuondoka kwanza na kurudi baadaye kuendelea kuzungumza kila mmoja anapokuwa katika nafasi nzuri ya kutumia vema akili yake.

  5. ZUNGUMZA NAYE KWA MUDA MUAFAKA

  Usianzishe mazungumzo magumu au makali na mwenzi wako kama hauko mahala muafaka na wakati pia si muafaka. Njaa na uchovu vinaweza kusababisha mtu kujibu hovyo au kutojali. Pia si vema kumuuliza jambo mwenzako iwapo mmoja au nyote mmepata kileo.

  Vilevile, epuka kuzungumzia masuala magumu ya kimahusiano iwapo jicho la pili litakuwa limeelekezwa kwenye kitu kingine. Zima TV, pia zima simu na laptop. Kama ulikuwa unasoma gazeti, lifunike ndipo uanze kuzungumza na mwenzako masuala nyeti ya kimaisha. Kama ukiona mazingira hayaruhusu, chagua wakati mwingine.

  Lakini pia, kabla hujaanza mazungumzo na mwenzako, jiulize iwapo hutasababisha rabsha. Jiulize, je, mazungumzo yetu yataisha kwa furaha? Kama utabaini kuwa yanaweza yasiishe kwa furaha basi acha na kupanga siku nyingine.

  6. TUMIA VEMA MASIKIO YAKO

  Jambo hili la mwisho ni muhimu sana katika kuimarisha uhusiano wa kindoa. Ukitaka kupunguza migogoro baina yako na mwenzako, jifunze kuzungumza kidogo na badala yake kuwa msikivu zaidi. Kauli za lawama, matusi, kukosoa na nyingine za aina hiyo hubashiri mwisho wa uhusiano. Na hata kama uhusiano hautaisha lakini ni rahisi ndoa kuwa ndoana.

  Mazungumzo yako na mwenzako yanapoanza kuchemka na kuonekana kama vile yanaelekea kubaya, epuka kumkata kauli mwenzako – iwe ni kwa kutoa suluhisho au kujitetea. Mwenzako anapokuwa na kitu kifuani, anataka kusikilizwa. Kwa hiyo msikilize na uoneshe kuwa unamsikiliza kwa kutikisa kichwa (juu-chini), au kumwitikia kwa mguno wa kumwonesha kuwa unamsikiliza na kuheshimu maneno yake.

  TIMIZA WAJIBU WAKO

  Iwapo utayazingatia mambo haya sita utakuwa umejenga msingi imara kwa mpenzi wako kuwa wazi kwako na kukupa mapenzi yote. Namna hii, japo ndoa yenu inaweza kupita kwenye misukosuko mara kwa mara, lakini itaibuka kidedea.

  NINI UNATEGEMEA KUTOKA KWA MCHUMBA WAKO/MWENZI WAKO?.
  Je, ni kweli kwamba ndoa ni furaha tu? Hakuna huzuni? Hakuna ugomvi? Rafiki zangu, hata viongozi wa dini, wanapofungisha ndoa, husisitiza kuhusu kuvumiliana, kutunzana na kupendana kwa dhati hata katika kipindi cha shida na raha.
  Kwa bahati mbaya, baada ya rafiki zetu wanapokea tofauti maneno haya, wanaamini kwa kuambiwa, humaanisha kwamba kupendana labda hata kama fedha ya kula itakosekana nyumbani, mwenzake akiumwa n.k. Huo ni mtazamo tasa. Katika mada hii nitakufumbua, ujue nini zaidi utakutana nacho ukiwa ndani ya ndoa.

  KWANINI TUNAJADILI?
  Rafiki yangu ipo haja ya kujadiliana juu ya jambo hili tena kirafiki kabisa. Haya ni mambo ambayo sisi vijana tunakutana nayo. Ni wazi kwamba, kila kijana anawaza kuhusu ndoa.

  Anawaza kuoa au kuolewa. Anatamani kuwa na familia yake ili aitwe mama au baba, au siyo jamani? Sasa kabla ya kuingia kwenye hizo ndoa ni lazima tuzijue kwanza, hii ndiyo sababu hasa iliyonisukuma kuandika mada hii.

  FIKRA ZA WENGI
  Kama nilivyoeleza hapo juu, fikra za wengi ni tofauti. Asilimia kubwa wanafikiria zaidi kuhusu maisha mazuri yasiyo na mikwaruzano. Wanawaza kufurahia ndoa na kudhani hakuna changamoto nyingine.
  Wapo wanaofikiria hata suala la tendo la ndoa. Kwamba watakuwa huru kukutana kila siku kadiri watakavyoweza kwa kuwa wapo pamoja ndani. Hii ni mitazamo mibaya sana katika ndoa.

  Ni kweli unaweza kufanya tendo la ndoa na mwenzako mara nyingi uwezavyo, lakini nani amekudanganya kwamba kila siku utaendelea kumuona kama umuonavyo leo? Amini usiamini, zipo ndoa nyingi zinazolalamikia suala la tendo la ndoa.
  Kuna ambao wanadai hawatoshelezwi huku wengine wakilalama kuwa wenzi wao hawataki kabisa kutoa unyumba. Unajua kwa nini? Ama ana mtu mwingine pembeni au amechoshwa na mapenzi ya aina moja kila siku.

  (i) Wanaume
  Hawa fikra zao huwa kwenye suala la usafi, wanaamini wakiwa kwenye ndoa nyumba itakuwa safi, nguo zitafuliwa, kupikiwa na mambo mengine ya kifamilia.
  Akili zao zinakomea hapo tu, hawawazi kuhusu migogoro na namna ya kutatua. Wanaota kuwa na maisha mazuri, kuwa na watoto na kujijengea heshima kwa jamii. Hilo tu, basi!

  (ii) Wanawake
  Baadhi ya hawa ninaowazungumzia hufikiria kuhusu kuvaa vizuri, kutolewa out, kupata watoto na mengineyo. Kamwe hawana muda wa kufikiria juu ya matatizo ambayo yanaweza kutokea katika maisha ya ndoa.
  Hili ni tatizo. Rafiki zangu, maisha ya ndoa hayana furaha siku zote. Kuna wakati dhoruba hutokea na kusababisha mifarakano hivyo kuhitajika umakini wa hali ya juu katika kumaliza tatizo. Si kila siku kuna amani.

  TATIZO LIPO WAPI?
  Kwa wale ambao wana mitazamo ambayo nimeeleza hapo juu, huwa hawana muda kwanza wa kuwachunguza wapenzi wao, lakini pia wao wenyewe kuonesha tabia zao halisi ili wenzi wao waweze kusoma kama wataweza kuendana nao.
  Rafiki zangu, kwa ujumla hatutakiwi kufikiria mazuri pekee kwenye ndoa, kuna mengi ya kuvumiliana. Lakini pia kabla ya kuamua kuingia kwenye ndoa na mwenzako, kipengele kifuatacho hapa chini ni silaha muhimu sana kwako.

  ISHI MAISHA YAKO HALISI
  Huwezi kumjua mwenzako kama atakuwa anaishi kisanii na wewe. Sikiliza, kwa wiki mnakutana mara mbili tu, tena mnakaa kwa muda usiozidi masaa mawili, si rahisi sana kuweza kujuana tabia zenu halisi.

  Pamoja na hayo, wataalamu wa mambo ya mapenzi wanashauri ili mwenzi aweze kuwa wazi zaidi kwa mwenzake ni vyema yeye akaanza kuwa wazi na kuishi maisha yake halisi kwa uwazi. Usijilazimishe kupenda kitu ambacho hukipendi. Kama kuna jambo ambalo analifanya na linakuboa, mwambie ajue ukweli.

  Kwanza, uwazi wako kwake utamfanya naye awe wazi kwako. Hatakuwa na sababu ya kuigiza maisha wakati wewe unaishi maisha yako halisi.

  Kila mmoja akimjua mwenzake, ndoa haiwezi kuwa na matatizo, maana kila mtu atakuwa anajua anaishi na mtu wa aina gani. Inawezekana kabisa, mmoja wenu akaona tabia za mwenzake zimemshinda. Kama ni kweli na umegundua kwamba kuingia kwenye ndoa ni sawa na utumwa, fanya maamuzi!

  NATAMANI sana kuona maisha ya vijana wa sasa yakiwa hayana migogoro, hasa ya mapenzi. Ni furaha yangu kuona vijana wakifanikiwa katika kazi zao na maisha yao kwa ujumla. Rafiki zangu, maisha bora au utaratibu mzuri wa maisha unatokana na uhusiano mwema wa mhusika na mwenzake.

  Kama ulikuwa hujui, leo chukua hii elimu, kijana/mtu ambaye amegombana na mpenzi wake usiku uliopita, siku yake huwa nzito sana kazini. Kila anachokifanya hukumbuka ugomvi wa usiku.

  Kama mtu ataondoka nyumbani akiwa hana maelewano na familia yake, ni wazi kwamba siku yake itatawaliwa na giza. Hata kama atajitahidi kuficha, lakini itafikia mahali atashindwa. Kazi inahitaji utulivu.

  Ndivyo ilivyo katika maisha, lazima upate mwenzi sahihi ambaye atakupa furaha badala ya mateso. Hapa ndipo tunapojadili jambo moja kubwa na muhimu sana; amani na furaha ya ndoa.

  Je, wewe unatarajia nini kwenye ndoa yako ijayo? Unahitaji mafanikio au kuvurunda kila siku kwenye biashara zako? Kama unataka kuwa bora, lazima pia uwe na mwenzi sahihi. Rafiki zangu wengi wanajiandaa kwa mazuri tu kwenye ndoa zao.
  Hawana mpango na changamoto na migogoro, hapo watakuwa wanakosea sana.

  Kama mnakumbuka vizuri, wiki iliyopita nilieleza kwanza sababu za kujadili mada hii, namna ambavyo baadhi ya watu wanawaza na tatizo lilipo, ambapo imeonekana wengi wanaishi na wapenzi wao kabla ya ndoa, maisha ya kuigiza tu! Yaani anaonesha tabia za ‘kupaka rangi’ lakini akishaingia ndani anabadilika.

  Kitu kikubwa ambacho nilikifafanua wiki iliyopita ni tabia ya kuishi maisha yako halisi bila kuigiza. Kufanya hivyo kutampa nafasi mpenzi wako naye aishi maisha yake ya kawaida, mwisho kila mmoja atamjua mwenzake.


  KEMEA MAPEMA MATATIZO
  Katika kuishi kwako maisha yako halisi, mwenzako naye atakuwa kama wewe. Hiyo ni hatua nzuri maana itakuwa rahisi sana kwako kugundua tabia za mwenzako. Hapo utazijua nzuri na mbaya.

  Acha kulea matatizo, bila kujali jinsi, mwambie mpenzi wako tabia ambazo hazikufurahishi. Ili aweze kubadilika kwa urahisi zaidi, unatakiwa kumwambia kwa utaratibu, lakini pia umpe sababu za wewe kukataa tabia zake hizo.

  Akiendelea nazo kuwa mkali, wakati mwingine ukali unasaidia. Kwa kukemea, kama ni kweli anakupenda na anahitaji uhusiano wenu uendelee, basi lazima atabadilika. Akifanya hivyo itakuwa vizuri zaidi kwako, maana utakuwa na uhakika angalau kwa asilimia chache kwamba mpenzi wako anakusikiliza.

  TABIA ZA ASILI
  Rafiki zangu, lazima ufahamu kwamba wakati unapambana na tabia za mpenzi wako zisizokupendeza, zipo tabia nyingine ni za asili. Hazibadiliki. Sasa hapo lazima uwe makini kwa mambo mawili; Mosi, zitakuathiri?

  Pili, ni tabia zitakazokugombanisha na jamii? Maana kuna tabia nyingine zinavumilika, lakini je, hazitaleta athari kwa majirani zenu watarajiwa? Haya ni mambo ya kuyatafakari kabla ya kuingia kwenye ndoa.

  Mathalani, kuna baadhi ya watu wana viburi au dharau za kuzaliwa! Hata umfanyeje, habadiliki. Unaweza kumwuliza kitu akanyamaza. Ni tabia ya kiburi, lakini kwa sababu amezaliwa akiwa na tabia hiyo, hawezi kuiacha. Sasa hapo lazima ujiulize, utawezana naye?
  Utaweza kumvumilia na kiburi chake kwa maisha yenu yote? Huu ni mfano tu rafiki zangu, zipo tabia nyingi za asili, ambazo kwa nafasi yako unaweza kuzichunguza kwa mpenzi wako kabla ya kuchukua uamuzi mzito wa kuingia kwenye ndoa.

  KUWA MKWELI
  Ukweli ni silaha, ni haki na siku zote humfanya mtu awe huru. Kama kuna jambo ambalo hujalipenda kwa mpenzi wako, haraka mwambie. Acha kukaa na vitu moyoni. Si utaratibu mzuri.

  Hata kama nguo zake hazikufurahishi mwambie: “Baby yaani kiukweli ukivaa hizo jeans zako hupendezi kabisa. Nadhani uanze kuvaa suruali za vitambaa.”

  Hapo utakuwa umemwambia ukweli wako, kukubaliana na wewe au kukataa kutatokana na mapenzi yenu wewe na yeye. Kama anakupenda atakusikiliza. Kwani anamfurahisha nani huko barabarani zaidi yako? Kuwa mkweli.

  UTARATIBU WA KAZI
  Suala la kazi kwa baadhi ya wanandoa huwa ni tatizo. Utakuta mwanaume amemkuta binti wa watu anafanya kazi, wamependana na kufunga ndoa. Ghafla anamwambia mwenzake aache kazi!

  Ndoa nyingi hasa changa huingia kwenye mgogoro huu. Kwangu mimi, wanandoa wote kufanya kazi ni bora zaidi, maana ile maana ya usaidizi wa mwanamke inakuwa imekamilika. Kwa maisha ya sasa mama kukaa nyumbani siyo ‘dili’ tena.

  Hata hivyo, ili kuepusha matatizo, suala hili ni vyema mkajadiliana mapema. Kaa na mwenzako, mwulize: “Lakini dady, vipi kuhusu kazi baada ya kufunga ndoa?”

  Anzisha huu mjadala na mwisho muwe na majibu yenye usawa. Mkubaliane kwa pamoja. Vijana wa mtaani wanasema, ‘kwa roho safi’. Hii itakusaidia maana mgogoro huu utakuwa umeisha kabla hata ya ndoa yenu.


  VIPI NDUGU ZAKE?

  Kama ni kweli una matarajio mazuri kutoka kwa mwenzako, kipengele hiki ni muhimu kabla ya kufanya uamuzi wa kuingia kwenye ndoa.

  Lazima uijue vizuri familia yake. Anatoka katika familia ya namna gani? Kabila gani? Ukiachana na hilo, hapa lazima ufahamiane na ndugu zake, japo kidogo na upate muda wa kuwazoea.

  Kuna familia nyingine ni wakorofi, kama ukiolewa huko ni tabu tupu. Pengine ukiona katika familia yao, labda wana tabia ya udokozi...si ajabu ukaibiwa hata wewe.
  Kweli umempenda na unataka kuishi naye, lakini utaratibu mbaya wa ndugu zake ni kielelezo cha matarajio ya maisha yenu ya ndoa. Kuwa makini.

  UNAIJUA AFYA YAKE?

  Baadhi ya watu kwa bahati mbaya wana matatizo ya kiafya ya kudumu. Utakuta huyu ana udhaifu wa kusumbuliwa na shinikizo la damu, mwingine vidonda vya tumbo, kifafa n.k.

  Ni udhaifu ambao yeyote anaweza kuwa nao. Kwa nini nimegusia hili? Kuna baadhi ya rafiki zangu wanaingia kwenye ndoa wakiwa hawajui matatizo ya wenzao, hivyo kusababisha usumbufu.

  Hujui mwenzako anasumbuliwa na nini, mnagombana kidogo unaanza kumpiga, unashangaa ameanguka chini, damu zinaanza kumiminika puani! Si kosa lako, maana hukujua!

  Hapa kuna umuhimu mkubwa sana wa kujua afya ya mwenzako. Kama ana maradhi ya kudumu ni vyema ukajua, ili pia ufahamu utakavyotakiwa kuishi naye ndani ya ndoa. Hakikisha unaijua historia ya afya yake vyema. Hakuna maana mbaya kufahamu, isipokuwa utakuwa na uwezo wa kumchukulia kulingana na udhaifu wake.

  MILA NA DESTURI

  Kuna makabila mengi nchini, kila watu wana mila zao, lazima uzijue japo kwa ufupi. Unaweza kuzungumza naye au ukawashirikisha watu wazima ambao wana ufahamu mkubwa, watakusaidia.

  Unaweza kuingia kwenye kabila ambalo mila zake zinaruhusu mwanaume kulala na shemeji yake kama kaka yake hayupo; itakuwaje hapo kama ulikuwa hujui?

  Kuna mengi ambayo siwezi kuyaandika yote, lakini jambo kubwa na muhimu kwako hapa ni kuhakikisha unafahamu mila na desturi za mume/ mke wako mtarajiwa.

  KUHUSU IMANI ZA DINI

  Inapendeza zaidi kama mkioana ndani ya imani moja ya dini. Upo utararibu wa wachumba kufunga ndoa bomani, ambapo kila mmoja huwa na dini yake. Siku za hivi karibuni wengi wanafanya hivyo, lakini si sahihi kwa asilimia mia moja.

  Ndoa imara, ukiacha juhudi za wahusika wenyewe hujengwa na hulindwa na imani thabiti ya dini ya wahusika. Mnapokuwa katika imani moja, ni rahisi kumfikia Mungu pamoja katika maombi au kwenda kwa viongozi wa dini pamoja na kupewa ushauri wa kiroho.
  Jambo hili lisiwe la mwisho, kama tayari dalili za kuoana zinaonekana wazi, muanze kujadiliana mapema juu ya suala la dini. Lazima muwe dhehebu moja, kama mpo tofuati, mshauriane ili mmoja amfuate mwenzake. Hakuna kinachoshindikana kwenye mazungumzo.

  MNIE MAMOJA

  Hapa namaanisha kwamba, ili ndoa yenu iwe bora lazima kuanzia mapema muwe na nia moja kwa kila jambo. Sina lugha nyepesi sana ya kudadavua hili, lakini kikubwa ni kwamba mnapaswa kuwa na mawazo ya aina moja kwa maana ya kushirikishana tangu mapema.
  Jengeni mazoea ya kushirikishana kila kitu. Hii itawajengea uaminifu na kila mmoja kujiona sehemu ya mwenzake.

  Kwa nini yote hayo?
  Ndiyo taswira ya kile unachokiendelea ndani ya ndoa. Ikiwa uhusiano wenu awali haukuzingatia niliyoyataja hapo juu, matarajio ya ndoa yako yatakuwa kinyume.

  Acha utaratibu wa kuamini kwamba kwenye ndoa kuna furaha, kuna starehe tu, kuna kusaidiana tu. Zipo changamoto ambazo lazima ukubaliane nazo au ujiandae kukutana nazo kuanzia mapema.

  Kwa hakika hayo yakifuatwa kwa makini, ndoa yenu itakuwa bora na bila shaka utakuwa na matarajio mema katika ndoa yako ijayo,

 3. #3
  Member
  Join Date
  Dec 2014
  Posts
  38
  Rep Power
  0
  Likes Received
  3
  Likes Given
  12

  Re: ELIMU YA MAHUSIANO, KARIBU.

  Asante, mchumba angu anatokea kabila korofi, ni mkorofi, mtata hatari, ana wivu sijapata kuona. Nashindwa kumuacha manake ananipenda sana na kunijali, yani huwa nawaza nikimuacha sitopata mwingine atayenijali kama yeye.

  Upendo hufunika mabaya yote jamani, ukamilifu ni wa Mungu tuu, sote tuna mapungufu

 4. #4
  Senior Member MV Salama's Avatar
  Join Date
  Jan 2014
  Location
  New York
  Posts
  1,880
  Rep Power
  8
  Likes Received
  104
  Likes Given
  80

  Re: ELIMU YA MAHUSIANO, KARIBU.

  Asante Da Kiboga,
  Wahenga walisema Mpende akupendaye nami nafurahishwa na neno hilo pia nakusihi mpende sanaaaaa huyo anayekujali usimuache aande zake coz
  "niafadhali ya ndege mmoja tunduni{kiotani} kuliko ndege mia mtini.
  Da Kiboga likes this.

 5. #5
  Member
  Join Date
  Jul 2014
  Posts
  30
  Rep Power
  0
  Likes Received
  0
  Likes Given
  3

  Re: ELIMU YA MAHUSIANO, KARIBU.

  Umemaliza kila ki2,sina la kuongezea

 6. #6
  Senior Member MV Salama's Avatar
  Join Date
  Jan 2014
  Location
  New York
  Posts
  1,880
  Rep Power
  8
  Likes Received
  104
  Likes Given
  80

  Re: ELIMU YA MAHUSIANO, KARIBU.

  karibu mkuu..

Posting Permissions

 • You may not post new threads
 • You may not post replies
 • You may not post attachments
 • You may not edit your posts
 •