KUBADILI TABIA NA KUJUA WAJIBU ZETU KAMA WAZAZI BORA.
UTANGULIZI.
Tunazungumza kuhusu wajibu wa mzazi kwa watoto katika malezi bora na yenye kuleta manufaa kwa Taifa ambalo ni jamii inayotuzunguka pamoja na Mungu.
MUHTASARI WA SOMO:
1. WAJIBU WAKO MZAZI KWA MTOTO KIJAMII.
(a) Haki za mtoto
(b) Wajibu zako ni zipi kama mzazi
Mtu mwingine asifanye wajibu wako kwa ajili yako:
Wajibu wa mazazi kumpatia mtoto mapumziko unapaswa kupewa msukomo wa kipekee. Ni wajibu ambao unachangia kukua kwa mtoto katika nyanja za kiutamaduni, kisaikolojia, uhusiano na ubunifu. Mtoto anapopata nafasi ya kucheza, kupumzika na kujifunza kuhusu mazingira yake na hasa masuala ya kiutamaduni hujifunza mengi ambayo hawezi kujifunza kwa namna nyingine.

Mtoto anapopata fursa hii ndipo anapoweza kubaini namna ya kutatua matatizo mbalimbali ya kibinafsi na kijamii. Wajibu huu ni jukumu la wazazi lenye lengo la kumjenga mtoto kiakili, kijamii, kimaadili, kiutamaduni na kisaikolojia. Hapo ndipo wajibu huu unapokuwa ni haki ya msingi ya mtoto.

Wajibu wa kumpatia mtoto elimu, afya, malazi na chakula unatokana na nafasi yetu kibinadamu, kijamii na kisheria. Wajibu huu hautegemei tu mapenzi ya mzazi kwa mtoto wake, bali uwepo wa miundobinu, mitazamo ya kijamii na uwezo wa kifedha au kiuchumi wa mzazi.

Wajibu huu ni vyema umeainishwa kisheria ili jamii ielewe kwamba siyo chaguo la mzazi, bali ni la msingi kabisa. Serikali ina jukumu kubwa la kuhakikisha siyo tu inasimamia utekelezaji wa wajibu huu, bali pia kuwawezesha wazazi na jamii ambayo haina uwezo wa kutekeleza wajibu huu.

Vilevile, pale inaposhindikana kutekeleza wajibu huu kutokana na upungufu wa kiutendaji, haina budi kuhakikisha vikwazo hivyo vinaondolewa ili mtoto aweze kufikia haki hii. Chini ya hapo, serikali itashindwa kusimamia kwa ufanisi utekelezaji wa wajibu huu.


Ukweli ni kwamba, pamoja na sheria kuwepo, watoto wenye wazazi walio na kipato kidogo au wasio na kipato kabisa, hawataweza kufaidi upatikanaji mzuri wa huduma hizi. Utekelezaji wa wajibu huu ni lazima uambatane na msukumo wa serikali wa kutimiza wajibu wake kwanza na kuondoa vikwazo vyote, viwe vya kimiundombinu, kiutendaji au kiuchumi.Wazazi wengi wanaweza kupuuza wajibu wao wa kumpatia mtoto heshima na utu. Ni vyema kuelewa ni kwa nini wajibu huu umeainishwa kisheria. Wajibu huu siyo tu msingi wa kufanikiwa kwa mtoto katika maisha, bali humjengea uwezo wa kujiamini na kujistahi.
Mtoto anayelelewa katika mazingira ya kutukanwa, kuteswa, kunyanyaswa, kutoheshimika au kushushiwa utu au hadhi yake kwa namna yoyote ile huwa na mtazamo hasi kuhusu uwezo wake wa kufikiri na kutenda.
Hupoteza uwezo wa kujithamini na kujiamini mbele ya jamii na hivyo kumsukuma katika matatizo mengine, ya kisaikolojia, kiakili na kiroho tangu umri wa utoto mpaka utu uzima. Matizo haya huleta athari kwa mtoto, familia na nchi kwa ujumla katika nyanja zote.
MAJADILIANO YA VIKUNDI JUU YA WAJIBU KIJAMII.
(a) Unatambua haki za watoto wako?
(b) Ulishawahi kusikia kuwa watoto wana haki?
(c) Nini matatizo au vikwazo vinavyozuia usitimize wajibu wako katika kutimiza haki za watoto wako?
(d) Tufanye nini kuondoa tatizo hilo?
HITIMISHO:
Kila mzazi anapaswa kuzitambua haki za mtoto kimwili, kijamii na kiroho ili kumuwezesha kumlea huyu mtoto katika njia inayofaa ambayo hata iacha hata atakapo kuwa mzee! Mithali 22:6 inavyosema.
2. 3. WAJIBU WAKO MZAZI KWA MTOTO KIMWILI.
HOTUBA YA WAZIRI MKUU KUHUSU WAJIBU WA WAZAZI KWA WATOTO.
“Wazazi wenzangu popote pale mlipo Tanzania jukumu la kuwalisha Watoto ni jukumu la kila Mzazi. Kwa mtazamo wangu mimi, na kama Mzazi, ninaamini kuwa Wajibu wa kwanza wa Wazazi, pamoja na mambo mengine, ni kuwalea na kuwakuza Watoto katika Maadili na Tabia njema. Katika kufanya hivyo, Wazazi wanao wajibu wa kuhakikisha watoto wanapata mahitaji yote ya msingi na muhimu kama vile Chakula Kizuri, Matibabu Mazuri, na Elimu Bora ili kuweza kukua kiakili na kimwili.”
4. HUSIKA NA WAJIBU WAKO KWA MANUFAA YAKO, TAIFA NA MUNGU.
Kumbuka mtoto ni taifa la kesho, linapaswa kujengwa katika msingi madhubuti na imara ili lisitetereke. Wazazi wengi wa sasa hawajali kufuatilia tabia za watoto wao, hawajishughulishi kujua wanaishi maisha gani, wana marafiki wa aina gani, wanapenda nini.
Badala yake wanawaacha wajiamulie na matokeo yake ndio tunarudi kulaumu nyimbo zenye kiitikio cha ‘Watoto wa siku hizi’, bila kujua kuwa sisi kama walezi wakuu, ndio tumewafanya wawe watoto wa siku hizi na sio wa zamani waliokuwa watii, wanaopendana na wanaosikia wakubwa. Wazazi wengi wanaowanyima watoto wao haki yao ya msingi ya malezi, na kuishia kuwatupia lawama. Ni jukumu na wajibu kwa wazazi kuhakikisha kuwa mtoto yeyote anapata elimu itakayomsaidia kimwili, kiroho na kiakili. Mzazi atakapoutekeleza vema wajibu wake kwa wanawe kwa kuwapa malezi yale ya kimwili na kiroho.
Utekelezaji huu wa wajibu utawajengea watoto hisia na mazingira ya kuwatendea wema wazazi wao na kuchunga haki zao. Kinyume chake, yaani mzazi atakapoacha kuutekeleza vema wajibu wake huo, itakuwa ni sababu itakayowapa watoto uhalali wa kuwatupa wazazi na kutowashughulikia watakapokuwa wakubwa. Utume kwa watoto lazima umjali mtu mzima, katika vipengele vyote. Malezi ya jumla kwa watoto (Holistic Child Ministry) ni kuwapa nafasi ya kujikuza kimwili, kiakili, kijamii, na kiroho. Kwa mantiki hii basi, kila kituo cha watoto kinatakiwa kuwa na nafasi ya kukuza vipengele hivi vinne vya binadamu. Kila kikundi cha watoto kufanikisha malezi ya jumla, kiwe na shughuli zinazoendana na mahitaji ya watoto kujikuza. Kwa hiyo, kituo kizuri cha watoto kinatakiwa kuwa na nafasi ya vipengele vifuatvyo. Tuzingatie kuwa vifuatavyo hapa chini havimaanishi sehemu ya majengo bali ni nafasi mbalimbali za kukuza mtu mzima. Pengine nafasi hizi zitaonekana katika ratiba na mazingira ya kituo.
· Uwanja wa mchezo unaowapa watoto nafasi ya kujiburudisha, na kutunza miili yao. Aidha, uwanja wa mchezo unawapa vijana namna ya kujenga mahusiano. Kwa hiyo, kituo cha watoto kinatoa nafasi za burudani, kama vile, mchezo, uimbaji, pikniki, n.k
· Darasa ambalo linawafundisha watoto maarifa mbalimbali, hivyo hukuza akili zao. Kikundi cha vijana kinawapa watoto mafundisho, na nafasi nyinginezo kama kusoma vitabu kwenye maktaba, kushiriki katika semina na warsha, kwenda kwenye safari za kielimu, n.k.
· Kanisa ambalo linawasaidia watoto kuunganika na Mungu. Sala, zilizoandaliwa vizuri na zinazochochea ushirikiano, majadiliano ya Biblia, retriti (mafungo ya kirohi), nafasi za kutenda matendo ya huruma, n.k. zinaweza kuwapa watoto fursa ya kujikuza kiroho.
· Nyumbani ambapo watoto wanajisikia kuwa wanakaribishwa. Wanajisikia kuwa wanapendwa na watu, na wanayo nafasi kujifunza namna ya kuzoena na watoto wenzao. Nyumbani hujengwa na watu. Kituo au kikundi cha watoto kinaweza kuwa nyumbani kama mlezi wa watoto anaweza kuwa karibu na watoto, kama rafiki, ndugu na mzazi. Usikivu wa watu wazima, na uwezo wa kutoa nasaha unageuza kituo cha watoto kuwa nyumbani.
Elimu ya Jumla (Integral Education)
Vilevile, hata shule zile zinazowajibika na ukuaji wa kiakili mahsusi, hutakiwa kujali vipengele vingine vya mahitaji ya wanafunzi. Hati maalumu iliyotolewa na UNESCO (Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa) mwaka 1996, kuhusu vipaumbele vya elimu katika karne ya ishirini na moja, inataja nguzo nne za elimu ya jumla:
1. Kujifunza kujua (Learning to know)
2. Kujifunza kutenda (Learning to do)
3. Kujifunza kuishi pamoja na watu (Learning to live together), na
4. Kujifunza kuwa (Learning to be)
Nguzo hizi za elimu zinaweza kutuelewesha zaidi kuhusu malezi ya jumla ya watoto
1. Kujifunza namna ya kujua:
Wajibu wa shule ni kukuza akili za wanafunzi kwa kuwapa maarifa. Lakini elimu si sawa na maarifa. Elimu ni ukuzaji. Ndiyo maana tunashauri kwamba shule inatakiwa kuwafundisha vijana watoto mbinu za kujifunza, kuliko kuwapa taarifa kadhaa ambazo vijana watoto hutakiwa kumrudishia mwalimu wakati wa mitihani. Bali elimu halisi hujenga hamu ya kujifunza daima, hata nje ya shule. Zaidi ya taarifa kadhaa, shule inatakiwa kuwafundisha vijana namna ya kuendelea na elimu hadi uzee (life-long education). Ndiyo, elimu ya shule ni maandalizi kwa ajili ya elimu ya maisha. Na elimu haina mwisho.
2. Kujifunza kutenda
Ujuzi peke yake hautoshi kuwakuza watoto. Wanahitaji utendaji. Elimu inaendana na ufundi stadi ambao huwawezesha watoto kufanya kazi fulani. Zaidi ya kuwaandaa watoto kwa ajili ya kufanya kazi, elimu huwaandaa watoto kukutana katika maisha yao ya kijamii, hali tofauti na ya shule. Kwa hiyo wanahitaji stadi za maisha, kama vile, kujitambua, kujithamini, namna ya kujenga uhusiano na watu, mbinu za kuwasiliana na watu, namna ya kukabili hasira na mshinikizo, jinsi ya kutatua matatizo ya maisha, n.k. Hivyo, elimu inawaandaa vijana watoto kwa ajili ya maish ya baadae.
3. Kujifunza kuishi pamoja na watu
Nyakati hizi za utandawazi tunazidi kuishi na watu wa makabila, lugha, mataifa, na desturi na mila mbalimbali. Ni wajibu wa wazazi kuwawezesha watoto kuishi na watu mbalimbali. Mtu mwenye elimu ni yule anayeweza kuelewana na watu tofauti na asili yao. Zaidi na zaidi watoto wanahitaji kupewa nafasi ya kuelewa historia, desturi na mawazo ya watu wa makabila na mataifa mbalimbali. watoto wanahitaji kuelewa kwamba njia ya kutatua matatizo kati ya watu ni kwa njia ya mawasiliano na majadiliano. Vita na mapigano hayana maana katika karne hii ya ishirini na moja.
4. Kujifunza kuwa
Mafanikio ya kweli ya mtu hayategemei na ujuzi alio nao wala stadi alizo nazo, bali yanategemea na hali ya nafsi yake mwenyewe. Elimu inatakiwa kujenga nafsi ya mtu. watoto wanahitaji kuelimishwa namna ya kuwajibika katika maisha yao; namna ya kuwa na msimamo dhabiti ya kimaadili; namna ya kutimiza ahadi za maisha yao; na namna ya kuwa raia wema na wakristu wazuri.
MAJADILIANO KATIKA VIKUNDI
1. Je unatimiza wajibu wako kama mzazi katika familia yako?
2. Taja baadhi ya maeneo ambayo unaona ni kikwazo cha wewe kutimiza wajibu wako kama mzazi
3. Nini kifanyike kukabiliana na tatizo au vikwazo hivyo?
HITIMISHO.
MAISHA YA MTOTO WAKO NA MSINGI ULIOMPATIA LEO NDIO UTAKAO WEZESHA MAISHA BORA YA MAMA NA BABA WA BAADAE!