NA LUQMAN MALOTO
Taifa la wanamasilahi, anga la burudani lilipambwa na kelele za umri wa Miss Tanzania. Yule binti aitwaye Sitti Mtemvu, eti ni mkubwa sana, ni mdanganyifu, alighushi nyaraka muhimu zinazohalalisha udogo wake tofauti na uhalisia.

Watu wakapaza sauti, eti Sitti, Hashim Lundenga ‘Anko’ na kamati nzima ya Miss Tanzania wameaibisha taifa kwa kitendo cha kumpa taji ‘bi mkubwa’. Kelele zilipigwa kila kona ya iitwayo mitandao ya kijamii. Haikushindikana, iliwezekana, binti kaachia taji. Unachezea kelele za umma?

Sipingani na vuguvugu lililosababisha Sitti kuachia taji la Miss Tanzania, japo sijaamini kama lilipopelekwa ndiko hasa njia kuu. Ila peke yangu nawaza, je, hivi aibu ya Sitti kudanganya umri, inafikia ile ya David Adedeji Adeleke ‘Davido’ kufanya shoo na kuondoka kurudi kwao salama?

Kwa nini kwenye Miss Tanzania kulikuwa na kelele nyingi lakini la Davido kuvunja sheria za nchi linanyamaziwa? Iweje Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) liingilie kati na kutia presha Sitti kuvuliwa taji ilhali limekuwa kimya kuhusu Davido kana kwamba halihusiki?

Vyombo vya habari kimya! Ni mwandishi gani ambaye hajui kama Davido alinyimwa kibali na Basata cha ‘kupafom’ Fiesta Oktoba 18, mwaka huu lakini pasipo woga, msanii huyo alipanda jukwaani na kufanya onesho? Je, waandishi hatujui habari?

Suala la Davido lilisababisha hata Mahakama ya Kisutu, kutoa hati ya Amri ya Zuio (Injunction Order) lakini bado mwanamuziki huyo wa Nigeria ‘alipafom’ na baada ya hapo ukimya umetawala. Nilijua ile adhabu ya kudharau mahakama (contempt of court) ingewakuta wahusika lakini wapi!

Amri ya Zuio iliyotolewa, ilipelekwa Jeshi la Polisi makao makuu, kisha Mkoa wa Kipolisi Kinondoni (Oysterbay) kwa utekelezaji lakini Davido alipanda jukwaani salama, bila kashkashi yoyote na baada ya hapo aliondoka kurudi kwao kana kwamba hakikutokea kitu.

Peke yangu nawaza; RPC wa Kinondoni, ACP Camillus Wambura, alingoja nini kumkamata Davido na waliompandisha jukwaani wakati tayari alishapewa Amri ya Zuio la msanii huyo ‘kupafom’ Fiesta 2014? Ukimya ule ulimaanisha polisi pia kuchekelea sheria za nchi kuvunjwa.

Kuna waandishi kadhaa ambao walikuwa mstari wa mbele kuandika suala la Sitti na tuhuma za udanganyifu, baadhi yao niliwauliza, kwa nini mashambulizi mengi Miss Tanzania (japo ipo hoja ya msingi) na vipi Davido ukimya umetamalaki utafikiri hakikutokea kitu?

Kuna ambao walisema suala la Davido haliandikiki kwa sababu lipo mahakamani (jawabu hilo lilinifanya nicheke). Wapo waliodiriki kutamka kuwa ‘ishu’ nzima ya Davido inalindwa kwa maelekezo ya wakubwa wa nchi (jibu hili liliumiza moyo wangu).

Kilichosababisha nicheke; mahakama haizuii vyombo vya habari kuripoti au kuchambua kilichopo mahakamani, isipokuwa inakataza uandishi au ripoti ambazo zitakuwa zinaingilia moja kwa moja mwenendo wa kesi na kutoa sura ya hukumu. Huko kunaitwa kuingilia uhuru wa mahakama.

Hata hivyo, suala la Davido lina namna nyingi ya kuandikwa na kuchambuliwa pasipo kuingilia uhuru wa mahakama. Hili lipo wazi kwa kila mwanataaluma wa kweli wa uandishi wa habari. Ila sishangai, maana wengi wanaandika kinachowavutia tu! Tena vyepesivyepesi ambavyo vinawafanya wasiitwe watata (controversial journalists).

SAKATA LA DAVIDO LINAANDIKWA BILA WASIWASI
Kwanza; suala la Davido linaweza kuchambuliwa kwa namna zote kupitia Basata peke yake. Kesi iliyopo mahakamani haiihusu Basata kwa namna yoyote. Mahakamani mlalamikaji ni Times Promotions and Entertainment, walalamikiwa ni Davido, Prime Time Promotion na kampuni ya HKN Music Ltd (inayomsimamia Davido).

Basata ni chombo cha serikali ambacho shabaha yake ni kukuza, kusimamia na kuratibu kazi zote za sanaa na wasanii. Kwa maana hiyo, baraza hilo haliingiliani na mahakama kwa sababu lipo kwenye mhimili tofauti.

Ni zaidi ya kichekesho kama tutaambiwa kuwa eti na Basata linashindwa kuchukua hatua stahili kwa sababu inasubiri hukumu ya mahakama. Hoja hapa inasindikizwa na alama ya kuuliza; yapo wapi meno ya Basata ikiwa maandishi yake hayaheshimiwi?

Ukimya wa Basata kwenye suala la Davido ni habari tosha. Hata hivyo, sijawahi kuona popote ambapo mwandishi wa habari amemfuata Kaimu Katibu Mtendaji wa Basata, kumhoji juu ya hatua ambazo baraza litachukua baada ya amri yao kupuuzwa.

Kama Davido alipafom katika mazingira ambayo Basata lilikataza, kwa hiyo kumbe inawezekana mtu yeyote kuleta msanii kutoka nje na kumpandisha jukwaani bila kibali na ikawa shwari tu! Hoja nyingine hapa ni kwamba kumbe serikali ipo mfukoni mwa watu.

Kuna swali lingine hapa; ule mkwara wa Basata wa kumshusha jukwaani msanii anayepanda kutumbuiza bila kuwa na kibali umeishia wapi katika sakata la Davido? Au siku Davido anapanda jukwaa la Fiesta walisahau kama walimnyima kibali?

Davido ni Mnigeria, alipafom na kuondoka huku akijua kuwa Basata iliinyima Prime Time Promotion kibali cha kumtumia mwanamuziki huyo kwenye jukwaa la Fiesta 2014. Vilevile kulikuwa na Amri ya Zuio la Mahakama ya Kisutu. Kwa kilichotokea, naye alikwenda kuwasimulia Wanigeria wenzake kuwa Tanzania mamlaka zipo kwenye mifuko ya watu.

Je, hatuoni kuwa hiyo ni aibu kubwa kwa nchi? Je, suala la raia wa kigeni kusimamiwa na kulindwa katika kuvunja sheria za nchi, linaweza kuwa dogo kwa lile la Sitti kufanya udanganyifu wa umri? Sasa kwa nini Sitti sana, ila Davido kimya?

Basata liliinyima kibali Prime Time Promotion kwa sababu tayari lilishawapa Times Promotions and Entertainment. Barua ya Kaimu Katibu Mtendaji wa Basata inasema hivyo. Kitendo cha Davido kupanda jukwaa la Fiesta siyo tu ni dharau kwa baraza, bali pia kuingiliwa kwa haki za msingi za Times.

Upande wa pili, sakata la Davido linaandikika kutoka mahakamani bila kuingilia uhuru wa mahakama. Mwandishi anapaswa kuweka somo lake liwe ukaidi wa Amri ya Zuio. Mahakama ya Kisutu inatakiwa kujibu swali juu ya nini kitafuata baada ya ukaidi wa Amri ya Zuio lake.

Amri ya Zuio ni tofauti na kesi ya msingi. Nitacheka pia kama nitaambiwa kuwa Mahakama ya Kisutu inashindwa kuchukua hatua dhidi ya wakaidi wa Amri ya Zuio kwa sababu kesi ya msingi bado haijamalizika. Kweli naapa, nitacheka mpaka nishikilie mbavu!

Kesi ya msingi inahusu mkataba. Times Promotions and Entertainment inawalalamikia Davido, Prime Time Promotion na HKN Music Ltd kwa makusudi kadhaa ya vitendo vya uvunjifu wa mkataba na vitendo vya kuinyima haki za kimkataba. Ndiyo maana katika makala haya sizungumzii kabisa mambo ya mkataba. Naheshimu sana uhuru wa mahakama!

HOJA KUHUSU WAKUBWA
Maneno kwamba kuna mkono wa wakubwa liliumiza sana moyo wangu. Taaluma yetu inaelekea wapi kama tutakuwa tunashindwa kuthamini nafasi zetu na kuacha wanaojiita wakubwa ndiyo watuamulie cha kuandika?

Mwandishi wa habari siku zote anapaswa kujitambua na kujipa thamani yake mwenyewe. Mwandishi wa habari ni bosi, maana kazi yake inaweza kumfanya mtu ang’are au apotee kama siyo kwenda na maji.

Uandishi wa habari ni taaluma inayoweza kuamua nchi iendeshweje. Katika uchaguzi inaweza kutamka huyu ndiye rais na akawa. Ikitumika vizuri, yenyewe ndiyo dawa ya maendeleo ya soka Tanzania. Inaweza kulipa thamani yake soko la muziki na kadhalika.

Mwandishi anapokuwa na habari yeye ndiye mkuu, wahusika wa ile habari wapo chini yake hata kama ni Rais wa Nchi. Muhimu ni kuzingatia weledi. Usitumie kalamu vibaya kuumiza wasio na hatia, vilevile kuwapa mng’ao na kinga wasiostahili.

Tatizo waandishi wengi hatujui thamani yetu, ndiyo maana wakati wa kuandika habari, ama inakuwa na woga mwingi au inaonea kama siyo kukandamiza upande fulani. Vilevile mwandishi anaweza kuigeuza habari au makala kuwa mapambio, yaani unampamba mtu mpaka kalamu inapoteza thamani.

Katika uandishi hutakiwi kuwa mwoga ila ni vema kuchukua tahadhari. Ukiwa mwoga sana hutafanya kazi yako barabara. Taaluma ya habari si rafiki wa wenye tamaa, maana rushwa huifanya kalamu ipinde. Aidha, unaruhusiwa kusifia lakini kuwe kwa haki. Linda thamani ya kalamu.

Hivyo basi, iliniuma moyo kuona waandishi wanashindwa kuchangamkia habari ya Davido eti kwa sababu ya uwepo wa maneno kuwa kuna wakubwa hawataki suala likuzwe. Nasisitiza, mwandishi ukiwa na habari ya kweli, tena ukweli ambao unaweza kuuthibitisha popote, wewe ndiye bosi mkuu, wote watakaokufuata wapo chini yako.

Ni imani yangu kwamba baada ya makala haya, waandishi tutaamka na kalamu zetu, kisha tuhoji pande zote zinazohusika ili kuufanya ukweli usimame kwenye vipimo vyake. Watanzania wanapaswa kujua; kwa nini Basata limedharauliwa? Iweje mahakama ipuuzwe? Na bila shaka huko mbeleni tutajua hao wakubwa ni akina nani.

By Luqman Maloto