Close

Results 1 to 2 of 2
Like Tree1Likes
 • 1 Post By Nakma Ahsam

Thread: ELIMU YA EDA

 1. #1
  Senior Member Nakma Ahsam's Avatar
  Join Date
  Jan 2014
  Posts
  164
  Rep Power
  6
  Likes Received
  16
  Likes Given
  8

  ELIMU YA EDA

  EDA - Hikma Yake, Hukmu Zake, Yanayopasa Na Yasiyopasa
  Familia-Wanawake

  Eda ni kipindi anachokaa mwanamke aliyeachika au aliyefiwa na mumewe, na baada ya kipindi hicho ndoa yake huwa halali. Na imeitwa eda kwa jina hili kutokana na jina la kiarabu ‘iddah’ kwa kukusanya kwake (idadi) ya miezi au ‘quruu’ [1] au hedhi au vipindi vya tohara ya hedhi.

  HEKIMA YA KUHALALISHWA EDA

  Hapa tunaona baadhi ya mawazo ya wanachuoni ambao wameona hizi ndizo hekima au sababu za kuwekewa eda shari'ah, ingawa hekima ya mwanzo na ya mwisho ni hiyo ya mwisho hapo chini ya fungu hili:

  Kutambua kama mwanamke ni mjamzito au la.


  Kuweza kubainika nasaba au kizazi ili kuepusha utata wa kutokujulikana nani ndiye baba.


  Kipindi ambacho mke anakaa eda kiwe kifupi au kirefu kinaangaza mwangaza wa kweli kuhusu uzito wa ndoa yao na mkataba mtakatifu walioufunga baina yao.


  Eda ya kufiwa inamwezesha mwanamke kutoa huzuni zake na kupata muda wa kujiliwaza na msiba uliomtokea wa kipenzi chake. Pia inamhifadhi kwa kutokuwa chombo cha kusemwa na kuzungumzwa kila apitapo.


  Kupata nafasi mume na mke kutafakari kwa makini kuhusu mahusiano yao kabla hawajavunja muungano wao wa kifamilia na haswa katika talaqa ivunjikayo (ya kwanza au ya pili)


  Ama HEKIMA ya juu kuliko zote kuhusu eda ni UTIIFU kwa maamrisho ya Mola wetu (Subhaanahu Wa Ta'ala). Kwani kuna wengi wanaotoa hoja za akilini mwao kama vile kudai kuwa siku hizi kuna utaalam wa kujua kama mwanamke ana mimba kwa vipimo bila haja ya kukaa eda mwanamke n.k. Hoja kama hiyo si ya busara maana ni sawa na kusema ‘siku hizi kuna kinga za mimba kama kondomu n.k, kwa hiyo zinaa iwe halali!’ Wamesahau kuwa HEKIMA kuu ni UTIIFU kwa Muumba na Utekelezaji wa MAAMRISHO yake na mengine ni ya ziada na wala si ya msingi. Allaah Anatujua zaidi kuliko tujijuavyo nafsi zetu.
  HUKUMU ZA EDA  1- Eda Kishari'ah

  Kishari'ah eda ina maana nyingi, mojawapo: Kupata yakini kwa kile kiumbe chenye kuzaliwa ili kuepukana na mchanganyiko wa nasaba. Na vilevile eda hekima yake hiyo eda ni kutoa fursa na muda kwa mume na mke baada ya talaka huenda kwa kipindi hicho wakamaliza tofauti zao na kurudiana na kuishi tena kama wanandoa kamili. Na pia sababu nyingine ni kulipa na kutekeleza haki haki zote za mume aliyefariki (ikiwa ni eda ya kufiwa) na kudhihirisha athari za kumpoteza mume, kwa kipindi cha maombolezi, nako ni kujizuia huyo mwenye eda na kujipamba, kujiremba n.k. kama tutakavyoona mbele.

  Na eda ni wajibu kwa mwanamke wakati anapoachana na mumewe, ima kwa talaka au kwa kufiwa na mumewe au ‘faskh’ (kutenguka kwa ndoa) au ‘khulu’u’ [2] (kujivua na ndoa hiyo). Na ni sharti awe ashaingiliwa na mumewe. Na eda haiwi kwa mwanamme, na anaruhusiwa kuoa mwanamke mwingine bila hata kusubiri kwisha hiyo eda ya mkewe. Ila tu kama kutakuwa na kizuizi, kama kutaka kumuoa dada ya mkewe, maana hairuhusiwi kishari'ah kuchanganya baina ya dada wawili kwa wakati mmoja kwani kishari'ah atakuwa yule mke aliyempa talaka ni wake hadi atakapomaliza muda wa eda yake. Au pia kama ana wake wanne na amempa talaka mmoja kati yao, haitoruhusiwa kwake kuoa mwanamke mwingine hadi eda ya huyo aliyemuacha imalizike vilevile. Kishari'ah hairuhusiwi kuwa na zaidi ya wake wanne.  2- Kumalizika Eda

  Kunatofautiana muda wa kwisha eda kutokana na sababu au aina za eda yenyewe. Aina zenyewe ni hizi zifuatazo:

  Eda ya aliyepewa talaka:
  Ni ‘quruu’ (vipindi vya hedhi/tohara) tatu, endapo atakuwa keshaingiliwa na mumewe na hakuwa ni mwenye mimba, au aliyekoma hedhi, au mdogo asiyepata hedhi bado. Na haya yamefafanuliwa na Allaah (Subhaanahu Wa Ta'ala) Aliposema: {{Na wanawake walioachwa wasubiri (wasiolewe) mpaka Twahara tatu ziishe…}} Al-Baqarah: 228

  Eda ya aliyefiwa na mumewe:
  Ni miezi minne na siku kumi, kama alivyoipangia Allaah katika Qur-aan: {{Na wale wanaofishwa (wanaokufa) miongoni mwenu na kuacha wake; hawa (wake) wasubiri (wasiolewe) miezi minne na siku kumi.}} Al-Baqarah: 234. Kiwango hiki ni endapo atakuwa si mjamzito (mwenye mimba), ama akiwa ni mjamzito basi eda yake itakwisha pale atakapojifungua. Kama tutakavyoeleza zaidi hapo mbele.

  Hakuna tofauti ya huyu aliyefiwa ikiwa mumewe alimwingilia alipokuwa hai au hakumwingilia, yote ni mamoja. Na atakapokufa mume na hali mkewe yuko katika eda ya talaqa rejea, itageuka eda hiyo na kuwa ni eda ya kufiwa. Ila endapo mume wa mke aliyeachwa talaka wazi atakuwa amekufa, na kumuacha kwake kulikuwa wakati akiwa na afya yake nzuri au kwa matakwa ya mwanamke mwenyewe, basi katika hali hiyo mke atakamilisha tu hiyo eda ya talaka na hatokaa eda ya kufiwa.

  Eda ya aliyekoma hedhi:
  (Kwa kupindukia miaka) Ni miezi mitatu kama Alivyosema Allaah: {{Na wale waliokoma kutoka hedhi miongoni mwa wake zenu, ikiwa mnayo shaka (katika muda wao wa eda), basi muda wao wa eda ni miezi mitatu…}} At-Twalaaq: 4. Na itakapowarejelea hedhi wakati ashaanza eda yake, basi atakaa eda ya ‘quruu’ badala ya miezi. Ama akiwa amepata hedhi mara moja au mbili tu kisha akawa katika hedhi yake iliyokoma basi arejee kwenye kukaa eda ya miezi mitatu badala ya ‘quruu’.

  Eda ya mjamzito (mwenye mimba):
  Inamalizika kwa kujifungua kama Anavyosema hapa Allaah (Subhaanahu Wa Ta'ala). : {{…na wanawake wenye mimba eda yao ni mpaka watakapozaa.}} At-Twalaaq: 4.

  Ama ikiwa mwanamke eda yake ishaanza naye hajui kama ana mimba na baadaye ikadhihiri hiyo mimba, basi atabadili eda yake kutoka kuwa ni eda ya ya mwezi na kuwa ni eda ya mimba (ujauzito). Na ataendelea na eda hadi atakapojifungua.

  Eda ya msichana ambaye hajafikia kupata hedhi, na eda ya mwanamke aliyevunja ungo ambaye pia hajawahi kupata hedhi na ambaye hakufikia umri wa kukoma hedhi:
  Hawa wote eda yao ni miezi mitatu kutokana na ushahidi wa maneno Yake Allaah: {{Na wale waliokoma kutoka hedhi miongoni mwa wanawake wenu, ikiwa mnayo shaka (katika muda wao wa eda), basi muda wa eda yao ni miezi mitatu, na (ndio muda wa eda kwa wale) ambao hawajapata hedhi bado.}} At-Twalaaq: 4. Lakini endapo itamtokezea hedhi mmoja kati ya wanawake wa aina hiyo kabla ya kumalizika muda wa eda yake, ataibadili hiyo eda na kuwa ni ya ‘quruu’ badala ya ile ya miezi iliyokuwa mwanzo.

  Eda ya mwanamke aliyezaa mapacha au zaidi:
  Itaanza baada ya kumzaa pacha wa mwisho, kwani mazingatio katika eda ya ujauzito ni kujulikana kiumbe (bara-atu rahim), kwa kuondokana kabisa na ujauzito.

  Eda ya aliyetowekewa na mumewe:
  Aliyetoweka ni yule ambaye hajulikani alipo na habari zake hazikusikika tangu alipoondoka au kutoweka pamoja na kutafutwa kwa muda mrefu. Wanachuoni wa shari'ah wametenganisha kati ya kupotea kwake kwa aina mbili: kujulikana alipo na kutojulikana. Ikiwa alipo panajulikana na ikiwa yuko salama huko alipo ima kibiashara, kikazi au kimatembezi, na kukakatika habari zake, basi wamesema wanachuoni kuwa ndoa yao bado itabaki hadi kuthibitike mauti yake au atoe talaqa au kupite muda mrefu ambao si wa kawaida ya yeye kupotea hivyo. Ikifikia hali hiyo, basi mke atakaa eda na kisha itakuwa halali kwake kuolewa tena. Ama ikiwa kupotea kwake kutajulikana kama vile kumesikika kuwa ndege aliyopanda katika safari yake imeanguka na hakupona mtu au gari alilosafiria limepinduka n.k, hapo mke atakaa eda ya mfiwa ya miezi minne na siku kumi. Na ikiwa kupotea kwake kumekuwa kurefu mno na hajulikani kama kapatwa na nini, na kukawa hakuna mawasiliano ya aina yoyote, basi hapo mke atasubiri kipindi cha miaka minne kisha atakaa eda ya mfiwa ya miezi minne na siku kumi. Ila ni vizuri zaidi kabla ya hivyo kuwe kumefanyika majuhudi makubwa ya kumtafuta kwa kutumia njia za kila aina na haswa kwa wakati huu ambapo njia za mawasiliano zimekuwa nyingi na nyepesi mno. Ni vizuri kutolewe taarifa kwenye vyombo vya habari, mitandao, mabalozi n.k.

  Lakini ikiwa kutoweka kwa bwana kukawa hatimaye kumebainika alipo na kukawa na mawasiliano, mathalan kumejulikana kuwa yuko jela na kifungo chake ni miaka mingi, au kasafiri mbali na atakawia sana kurudi, hapo kutatazamwa kama muda huo mrefu utamuathiri mke na watoto wake ima kiuchumi au kimwili au kiusalama, basi hapo mke ana haki ya kusubiri au kudai talaqa au kuomba kuachishwa na mume huyo. Qaadhi au Shaykh au Imaam au kiongozi wa dini ataangalia sababu za pande zote na dharura iliyopo kabla ya kumwachanisha mke na mumewe.  3- Yanayopaswa Kwa Mwenye Eda

  Wanachuoni wengi wa kishari'ah wamekubaliana kuwa mwenye eda anapaswa kukaa katika nyumba ya ndoa kwa muda wa eda yake yote hadi itakapomalizika. Ikiwa eda hiyo ni ya talaqa au ya kuomba kuachwa (kuachishwa) au ya kifo, haitakikani atoke ila kwa haja maalum au nyudhuru za kishari'ah la sivyo atakuwa ametenda dhambi. Na mume anaweza kumkataza asitoke ikiwa eda hiyo ni ya talaka, na mrithi ana haki ya kumzuia kutoka ikiwa eda hiyo ni ya kufiwa. Ila baadhi ya wanachuoni wanasema kuwa katika eda ya kufiwa mke anakaa eda yake atakavyo.

  Na inapaswa kwa mwenye eda ya kufiwa akae katika maombolezi (al-ihdaad) kwa muda wote wa eda yake. Na kuomboleza ni kuacha yeye kujipamba kwa mavazi ya marembo rembo, kuvaa dhahabu, na kujipaka manukato n.k. Kufanya hivyo kuna maana ya kuchunga na kuheshimu ule uhusiano wa kindoa uliokuwa baina yake na mumewe, nako pia ni kuonyesha utiifu kwa uhusiano wao. Pia kunapatikana katika huo muda wa maombelezi, utulivu wa nafsi ya mwanamke na kufikiria maisha mapya ya ndoa yamkabiliyo mbeleni.

  MAMBO MBALIMBALI KATIKA EDA NA HASWA EDA YA KUFIWA

  Haya ni baadhi ya mambo ambayo ni haramu kwa mwenye eda kuyafanya kishari'ah:

  Kujitia manukato mwilini au nguoni.


  Kujitia rangi za mdomo, rangi za kucha, poda, na aina zote za vipodozi.


  Kujitia wanja wa macho bila dharura ya kuumwa.


  Kuvaa nguo za rangi rangi: au ya rangi moja lakini yenye kuvutia na yenye mapambo. Si lazima hata hivyo kuvaa kaniki kama inavyodhaniwa na wengi au shuka la bafta n.k.


  Kuvaa mapambo ya dhahabu, fedha, lulu, almasi na madini mengine, ikiwa ni pete, mkufu, hereni, bangili na vinginevyo.


  Kujitia hina popote maungoni panapoonekana na watu.


  Kutoka nje pasipo na dharura. Haikatazwi mwenye eda kutoka nje kama hana wa kumtegemea kwa mahitaji yake, mathalan ikiwa inambidi kufanya kazi kwa kupata mahitaji yake, kwenda kununua mahitaji yake ya nyumbani, au kufundisha kama mwalim n.k.


  Kuolewa


  Kuposwa
  Nng'onda likes this.

 2. #2
  Member Nng'onda's Avatar
  Join Date
  Dec 2013
  Posts
  35
  Rep Power
  0
  Likes Received
  3
  Likes Given
  6

  Re: ELIMU YA EDA

  shukran kwa elimu nzur
  Utamu wa maharage hauwezi kuwa tofauti bali ni upishi wako tu

Posting Permissions

 • You may not post new threads
 • You may not post replies
 • You may not post attachments
 • You may not edit your posts
 •