Tangu asubuhi kumekuwa na habari inayosambazwa mitandaoni (ikinukuu chanzo kuwa ni Gazeti la Nipashe) ikidai kuwa Mwanasheria Mkuu wa Chama, Tundu Lissu (Mb) anatarajiwa kurejea nyumbani Tanzania wakati wowote kuanzia juzi, kwamba amemaliza matibabu yake.

HABARI hiyo si ya kweli. Imetungwa na walioitunga kwa sababu ambazo zinastahili kutiliwa shaka.

Uhakika ni kwamba Mwanasheria Mkuu wa Chama Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, hajazungumza na mwandishi yeyote wa Gazeti la Nipashe au BBC tangu amefika Ubelgiji kuendelea na awamu nyingine ya matibabu yake akitokea Hospitali ya Nairobi, nchini Kenya.

Uhakika mwingine ni kwamba AG Lissu hajazungumza na mwandishi wa habari yeyote juu ya kurejea kwake nyumbani kwa sababu zilizo wazi kabisa kuwa bado hajapona na anatarajiwa kufanyiwa upasuaji mwingine mwisho wiki hii au wiki ijayo.

Tunatoa wito kwa WanaChadema wote na Watanzania wote wenye mapenzi mema ambayo kutokana na kuguswa na uzito wa masahibu yaliyompata AG Lissu wameendelea kuguswa na kufuatilia kwa ukaribu maendeleo ya matibabu na hali ya afya yake, KUPUUZA uzushi huo.

Tunawasiliana na Dawati la Uhariri la Gazeti la Nipashe ambalo linatajwa kuwa ndiyo chanzo cha habari hiyo inayosambazwa mitandaoni, huku pia Gazeti hilo likiwa na habari yenye maudhui hayo ukurasa wake wa mbele, toleo la Aprili 30, 2018, ili kupata taarifa za kina juu ya kusudio la habari hiyo ambayo ni wazi imepotosha na kuleta usumbufu mkubwa katika jamii, ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA