Ni nadra sana katika Taasisi za Elimu ya Juu kutokea haya yanayotokea katika Chuo cha Ufundi Arusha. Ni muda mrefu sasa, toka menejimenti ya Chuo hiki ilipobuni mbinu za kufanya wanafunzi wasilalamikie chochote katika menejimenti hii pale ilipoona njia pekee ni kuongeza maksi (kiwango cha ufaulu) ili kuwafanya wasilalamike kwa lolote linalotokea dhidi yao.

Baada ya wanafunzi katika idara Fulani Fulani kugundua kuwa wamekuwa wakifundishwa bila kufuata mitaala inayokubalika na NACTE, au iliyopitwa na wakati bila kuuhishwa, nao wamebuni njia mbadala ya kuibana menejimenti ya Chuo kuwaongezea maksi kwa hoja kuwa wanafundishwa bila kufuata utaratibu unaokubalika na NACTE. Mara nyingi wamekuwa wakitishia kuifikisha menejimenti na Uongozi wa Chuo kwa Wizara ya Elimu kwa kile wanachodai kutokutendewa haki kama wenzao wa Vyuo vingine, pale ambapo wanafunzi hao wanajikuta wanafeli somo fulani. Baada ya menejimenti kubanwa na wanafunzi na kukubaliana na ukweli kwamba Chuo kimekuwa kikiendesha Taaluma isiyo na viwango kwa kutofuata curicullums zilizopitishwa na NACTE, Uongozi wa Chuo umekuwa ukilazimisha waalimu katika idara nyingi kuwaongezea wanafunzi maksi.

Mkuu wa Chuo Mr/Dr Richard Masika Mushi na Makamu wake Dr Masudi Senzia mara nyingi tokea hapo wamekuwa wakihubiri Filosofia yao isemayo SERIKALI KWA SASA INAJALI QUANTITY NA SIO QUALITY na hivyo kuwalazimisha waalimu kuongeza maksi kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayefeli. Waalimu wanaogoma kuwaongezea wanafunzi maksi wamekuwa maadui wa menejimenti na kuambiwa wanazorotesha ustawi mzuri wa Chuo. Na hata wanafunzi wamekuwa wakiambiwa wazi na menejimenti kuwa mwalimu wenu fulani ndiye hataki mfaulu. Kuhakikisha kuwa menejimenti inawabeba wanafunzi, makamu mkuu wa Chuo Taaluma amekuwa akichati na Wanafunzi ambao ni marafiki zake, na kuweza kujua mitihani ambayo wao (wanafunzi) wanahisi itakuwa migumu na kwa kufanya hivyo mara nyingi amefanikiwa hata kubadili mitihani iliyokuwa ifanyike na wanafunzi hao ili kuhakikisha wanafaulu.

Hali hii imewafanya hata baadhi ya wanafunzi, kuwa hawahudhurii madarasani kama inavyotakiwa kwa kile wanachoamini kuwa wakiona hali ni mbaya wataibana menejimenti kuongezewa maksi, na mara nyingi menejimenti imeweza kutii amri ya wanafunzi. Hali hii imeongeza kitu kama dharau kwa wanafunzi dhidi ya waalimu, kwani hata mwanafunzi asipoingia darasani, mwalimu anajua tu kuwa hana haja ya kumbana na kwamba hata akimbana mwisho wa siku mwanafunzi huyo atabebwa na uongozi na hivyo kuleta uhasama kati ya mwalimu na mwanafunzi.

Mara nyingi kitaaluma, wanafunzi wasiotimiza asilimia zinazokubalika katika mahudhurio ya vipindi vya darasani (Attendence) huwa hawaruhusiwi kufanya semester examination. Wanafunzi wa aina hii wamekuwepo wengi hapa Chuoni lakini pindi mwalimu unapopeleka request kwa (registrar na examination officers) kuwa mwanafunzi X asifanye Semester examination kwa kuwa haudhurii darasani utaambiwa sawa, lakini siku ya siku utamuona kwenye huo mtihani wako. Cha ajabu ni kwamba ukiendelea kukomaa kwamba usisahihishe paper yake, uongozi wa Chuo umekuwa ukiwapa watu wengine kusahihisha paper hiyona mwanafunzi kufaulishwa maana wewe mwalimu husika hutajua chochote na Kinachofuata ni chuki na dharau kwa mwanafunzi dhidi ya mwalimu husika. Hii ndio hali halisi iliyoko Chuo Cha Ufundi Arusha. Mara nyingi huwa waalimu tunajiuliza nia hasa ya uongozi wa Chuo kufanya hivi ni nini. Hivi wazazi wa wanafunzi hawa wanajisikia vipi wanapofikiri watoto wao wanafaulu kihalali, kumbe wanaongezewa maksi. Uongozi huu unadhalilisha wazazi na waalimu.