Ni katika hali isiyotarajiwa na inayokatisha tamaa Waalimu hapa Chuoni. Hivi karibuni wanafunzi walioko katika idara za Ujenzi na Barabara walitishia kuandamana na kwenda Wizara ya Elimu kwa kile walichodai kufundishwa na kutainiwa bila kufuata mitaala iliyodhibitishwa na kuidhinishwa na Baraza la Elimu ya Ufundi NACTE.
Ni baada ya wanafunzi wapatao 22, kujikuta wamefeli na kupata alama za chini ambazo kimsingi haziwaruhusu au zinawataka kurudia mtihani au kurudia mwaka. Wanafunzi hao baada ya kuona hivyo walianza kutafuta jinsi ya kujinasua katika hali hiyo, na kuitaarifu menejimenti ya Chuo Hiki nia yao ya kwenda kumweleza Waziri wa Elimu juu ya kile ambacho kinaendelea kwa sasa ambapo kila mwalimu anafundisha kitu ambacho anajisikia yeye, kwa vile Chuo kwa Muda sasa hakina mitaala iliyoidhinishwa na Baraza la Elimu ya Ufundi NACTE.
Menejimenti ya Chuo ililazimika kumuita mmoja wa waalimu, ambaye inaonekana somo lake ndilo lililoongoza kwa kufelisha na kuombwa aangalie jinsi ya kuwasaidia wanafunzi hao ili dai lao hilo lisije kufika kwa wakubwa kwani ni kweli mitaala inayotumika imepitwa na wakati na mingine imeandikwa tu hapa Chuoni bila kupelekwa NACTE kupata kibali, na kujikuta inatumika, hali inayofanya kila mwalimu kufundisha na kutaini anachotaka.
Mwalimu huyo alikataa, na kudai kuwa hata hizo alama walizopata baadhi ya wanafunzi hao, alilazimika kuziongeza ili kuwapa unafuu lakini bado walijikuta katika alama za chini. Baada ya mwalimu huyo kugoma menejimenti ya Chuo ililazimika kufanya kazi hiyo yenyewe kwa kile walichodai wao wanayo mamlaka ya kufanya hivyo kwa manufaa ya Chuo kwa wale wasiotakia Chuo mafanikio, na hatimaye waliwaongezea wanafunzi hao alama hizo na kuwafanya waweze kufaulu.
Inadaiwa baada ya kuona hivyo, Menejimenti ya Chuo hiki ilimtaka Mkuu wa Idara ya Ujenzi kutafuta mitaala iliyokuwa inatumika na ya zamani na kujitahidi kufanya kila kinachowezekana ili iweze kupelekwa NACTE, na hatimaye mitaala hiyo isiyokuwa na viwango tayari imeshapelekwa NACTE ili chochote kitakachotokea ielezeke kuwa tayari mitaala hiyo ilisha pelekwa NACTE kwa nia ya menejimenti hiyo iweze kujiondoa kwenye lawama hizo kirahisi.
“Siyo idara ya Ujenzi tu ambayo ina matatizo ya kutumia mitaala iliyopitwa na wakati, bali kwa sasa ni idara zote hapa chuoni kwani waalimu tunachapia-chapia tu kile mtu anachoona kinafaa” alisikika akisema mwalimu mmoja katika maeneo ya kantini wakati wakiendelea kupata chai ya saa nne.
Itakumbukwa kuwa mara nyingi wenye nia njema wametoa malalamiko yao kwa vyombo husika juu ya hali nzima ya Taaluma inavyovurundwa na menejimenti ya Chuo hiki. Katika hali isiyokuwa ya kawaida mwanzoni mwa semester hii, Mkuu wa Chuo, Mkuu wa idara ya Ujenzi na Waalimu wote waliondoka Chuoni kwa muda wa wiki tatu mfululizo na kwenda kuhudhuria semina Morogoro huku wakiwaacha wanafunzi solemba kwa wiki zote tatu bila kufundishwa. Haieleweki hizo wiki tatu ambazo wanafunzi hao hawakufundishwa zitahesabikaje au itakuwaje kwa kuwa watakuwa wamefundishwa kwa muda wa wiki 12 tu. Bila shaka watapewa alama za bure, kama ambavyo menejimenti ya Chuo hiki imezoea. Yetu macho.
Connect With Us