SHIRIKISHO la Soka Barani Ulaya (Uefa) limetoa ratiba ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, baada ya droo iliyochezeshwa leo mapema. Katika ratiba hiyo, Manchester City ya England watamenyana na PSG ya Ufaransa, mabingwa watetezi, Barcelona watamenyana na wapinzani wao wa la Liga, Atletico Madrid, wakati vigogo wengine wa Hispania, Real Madrid watamenyana na Wolfsburg ya Ujerumani.

Bayern Munich ya Ujerumani watamenyana na Benfica Ureno katika Robo Fainali ya mwisho ya Ligi ya Mabingwa mwaka huu.

Barcelona imeifunga mara zote mbili Atletico Madrid katika La Liga msimu huu, 2-1 kila mechi na mchezo wao unatarajiwa kuwa Robo Fainali tamu zaidi ya zote za Ligi ya Mabingwa mwaka huu.

Mechi za Robo Fainali zinatarajiwa kuchezwa Aprili 5 na 6, wakati marudiano yatakuwa Aprili 12 na 13.