Hatimaye rufaa ya wanamuziki maarufu nchini, Nguza Viking ‘Babu Seya’ na mwanaye, Johnson Nguza ‘Papii Kocha’, imesikilizwa katika Mahakama ya Haki za Binadamu Afrika (AfCPHR) jijini Arusha Machi 11, mwaka huu na sasa zimebaki saa 72 tu kujua hatima yao, yaani Machi 18, 2016,

Rufaa hiyo ilisikilizwa na mahakama hiyo yenye majaji 11 kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) ambapo rais wao ni Jaji Augustine Ramadhani wa Tanzania ambaye pia aliwahi kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania.MAJAJI WENYE SIRI MOYONI
Baadhi ya majaji waliotajwa kusikiliza rufaa hiyo na nchi zao kwenye mabano ni Ben Kioko (Kenya), Solomy Balungi Bassa (Uganda), Duncan Tambala (Malawi), Angelo Vasco Matuse (Msumbiji), Sylvain Ore (Ivory Coast), El Hadji Guisse (Senegal) na Rafaa Ben Achous (Tunisia).

KUTOKA MAHAKAMANI

Kwa mujibu wa chanzo cha uhakika kutoka katika mahakama hiyo, rufaa hiyo ilisikilizwa kwa faragha na hakuna mwandishi wa habari yeyote aliyeruhusiwa kuingia kupata mwenendo.
Chanzo kilizidi kusema kuwa rufaa ya mwanamuziki huyo na mwanaye, ilisikilizwa kwa karibu saa tatu tangu ianze na matokeo au hukumu wanayo wahusika.

SABABU ZAFICHWA

Hata hivyo, si Rais wa Mahakama ya Afrika, Jaji Ramadhani au mtu mwingine yeyote aliyeeleza sababu za kesi ya Babu Seya na mwanaye Papii Kocha isikilizwe faragha.

HATA JAJI RAMADHANI HAJUI

Wakati akichukua madaraka ya urais wa mahakama hiyo, Jaji Ramadhani alisema: “Kesi yoyote inayohusu nchi yangu mimi sitakiwi kuhudhuria kutokana na sheria zetu za mahakama hii…”
Kutokana na maneno hayo, kumezuka utata kwani haikujulikana mara moja kama wakati shauri la Babu Seya na mwanaye linasikilizwa, Jaji Ramadhani alikuwepo au la kwani rufaa ilipitiwa kwa faragha na kama alitoka nje basi itakuwa imepitiwa na majaji 10.

WATOA UAMUZI

Habari zaidi zinasema kuwa mara baada ya rufaa hiyo kupitiwa na majaji hao, shauri lao linapelekwa kwenye Kamisheni ya Afrika ya Haki za Binadamu ambako huko ndiko kutakakotolewa uamuzi ndani ya saa 72 zijazo.

WANACHODAI

Wanamuziki hao wamekata rufaa dhidi ya adhabu waliyohukumiwa mwaka 2004 ya kutumikia kifungo cha maisha jela ambapo mpaka sasa, wapo Gereza la Ukonga, Dar wakitumikia kifungo chao.
Kupitia shauri lao lililowasilishwa mahakamani na jalada lake kupewa namba 006/2015, wawili hao wanaiomba mahakama hiyo kutoa uamuzi kuwa haki zao zilikiukwa na wanaomba waachiwe huru na kulipwa fidia.

Pia wanataka mahakama hiyo iteue wataalam watakaotoa ufafanuzi wa hoja za kesi yao na kuisaidia kufikia wajibu wake.
Miongoni mwa hoja za Babu Seya na mwanaye zilizosikilizwa mahakamani hapo, ni pamoja na kwamba mwenendo wa shauri lao haukufanyika kwa kuzingatia haki, vilevile wanadai hati ya mashitaka dhidi yao ilikosewa kuandikwa tarehe ambayo tuhuma za makosa yao zilidaiwa kufanywa hivyo wakashindwa kutayarisha utetezi wao.
Pia wanadai mahakama iliyowatia hatiani, ilijielekeza katika ushahidi wa upande wa mashitaka pekee usioshirikisha ushahidi mwingine.

WANAISEMA SERIKALI

Wanadai kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia maofisa wake, ilivunja misingi ya haki za binadamu na sheria za kimataifa kwani ilivunja Ibara 1, 2, 3, 5, 7(1) b, 13 na 18 (1) ya Mkataba wa Afrika wa Ubinadamu na Haki za Binadamu.
Wanadai kwamba mashitaka dhidi yao yalitungwa na hivyo hukumu iliyotolewa haikujikita katika ushahidi wenye nguvu katika sheria.