Ray C ameweka wazi kuwa yuko taabani kiuchumi, hali inayompelekea kukosa hata pesa ya usafiri wa kwenda hospitali kupata dozi ya tiba ya maradhi yanayomkabili kutokana na kuathirika na matumizi ya dawa za kulevya.

Akiongea na Planet Bongo ya EATV hivi karibuni, Ray C alieleza kilio chake akidai kuwa sio tu kwamba amekosa pesa ya kuendelea kusapoti muziki wake baada ya aliyeahidi kumsaidia kumkimbia, bali inamlazimu kupanda daladala akiwa ndani ya vazi la ‘ninja’ kutokana na kushindwa gharama za usafiri.

“Jamani kiukweli haya maisha ya wasanii nyie acheni tu, yaani inabidi tumuombe tu mungu, mtu akikuona msanii kwenye daladala nani atanunua albamu yako, nani atakuja kwenye show yako, lakini mama ananiambia vaa ninja mwanangu nenda kapate tiba.* Kwa sababu kila siku kukodi taxi ni gharama sana, kutoa elfu 25,000 kutoka Bunju mpaka hospitali kila siku ni nyingi sana," alieleza.

“Sometimes namwambia mama inabidi tutoke mapema saa 11 hivi nivae ninja twende kwanza kanisani then naweza nikachukua hata bajaji kwenda hospitali. Haya ni maisha sio kitu cha kucheka ni lazima nifanye hivyo ili niweze kumaliza dozi,” aliongeza.

Ray C alieleza kusikitishwa na namna ambavyo baadhi ya magazeti yanamuandika na kumchafulia jina kwa kile alichodai ni habari za kutungwa kuwa amerudia dawa za kulevya, badala ya kuandika habari njema zinazomhusu.

Mwimbaji huyo ambaye album yake imekwama studio, aliwaomba wadau na wananchi kwa ujumla kumsaidia hata kwa kumchangia kiasi kidogokidogo cha fedha ili aweze kumudu gharama za maisha na hata kurejea jukwaani.
==